Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, Jumatatu tarehe 8-Agosti 2004
2 Agosti 2004Wakati wa ziara yake nchini Poland, kansela Schröder ameyakana wazi madai ya fidia ya Wajerumani waliofukuzwa nchini humo. Gazeti la Belin, DIE WELT, limeandika:
"Kansela Schröder alichagua maneno yanayostahili kuonyesha msimamo wake. Bila kupindisha maneno, alitamka wazi kwamba, madai ya fidia ya Wajerumani waliofukuzwa kutoka Poland si ya msingi.
Hata hivyo hotuba yake ilikosa mguso fulani wa nyoyo za watu walioathirika na maovu ya miaka iliyopita. Kinyume na walivyozungumzia jambo hili makansela waliomtangulia kama vile Brandt, Schmidt na Kohl, yeye hakuwa na maneno ya unyenyekevu kiasi cha kuwaingia watu akilini na kuwagusa nyoyo zao."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la DIE WELT.
Kuhusiana na mada hii, gazeti la OST-THÜRINGISCHE ZEITUNG limeandika:
"Gerhard Schröder alisema wazi, nani alianzisha vita, na nani ndiyo walikuwa wahanga wakubwa wa vita hivyo. Madai ya fidia kutoka kwa Wajerumani ambayo yanaweza kupindua historia, aliyapinga bila kusita. Ni wazi kwamba, uamuzi huu hautaungwa mkono na baadhi ya watu hapa nchini Ujeurumani. Hii ni kwa vile bado kuna watu wanaotaka kufuta maovu ya wajerumani wakati huo, kwa kisingizio cha makosa yaliyofanywa na nchi kama Poland -- Makosa ya kuwafukuza Wajerumani kutoka kwenye maeneo waliyokuwa wanayakalia. Ni kweli kwamba, vitendo hivi navyo havikuwa sahihi. Lakini, hii leo, miaka 60 baadaye, muda umefika wa kutumia busara na kuacha chuki hizo."
Nalo gazeti la ESSLINGER ZEITUNG limeongezea kwa kuandika:
"Miaka 60 baada ya maasi ya Warsaw, kansela Schröder amewahakikishia wananchi wa Poland kuwa, madai ya fidia kutoka kwa wajerumani ni yatu wachache tu.
Itakumbukwa kuwa, kansela Schröder ndiye aliyefanikisha hata malipo ya fidia kwa wafungwa waliofanyishwa kazi kwa nguvu wakati wa vita vya pili vya dunia."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la ESSLINGER ZEITUNG.
Gazeti la MANNHEIMER MORGEN limejihusisha na uhusiano kati ya Ujerumani na Poland, kwa kuandika:
"Historia tete kati ya nchi hizi mbili bado inawaelemea wananchi wa nchi hizi mbili. Wapolo hawawezi na hawataki kusahau maovu yaliyofanywa dhidi yao na utawala wa kinazi wa Ujerumani. Kwa kuangalia juujuu, wananchi wa Poland bado wana wasiwasi na Wajerumani. Lakini kwa upande mwingine, Poland na Ujerumani ziko mbioni kuachana kabisa na picha mbaya ya zamani.
Kitendo cha Kansela Schröder kupewa nafasi ya kutoa hotuba kwenye siku ya kuadhimisha maasi ya Warsaw, ni ishara nzuri kwamba, nchi hizi mbili zinataka kusameheana. Ushirikiano kati ya Poland na Ujerumani ndiyo kwanza umeanza."
Hayo yamendikwa na gazeti la MANNHEIMER MORGEN.
Mada muhimu ya pili kwenye magazeti ya Ujerumani leo hii ni makubaliano ya soko huria yaliyofikiwa kwenye mkutano wa shirika la biashara duniani, WTO. Gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND limeandika:
"Hatimaye majadiliano makali kati ya wawakilishi wa nchi 147 mjini Geneva yamekuwa na mafanikio kwenye upande wa soko huria. Wahusika wamekubaliana jinsi ya kufungua masoko duniani. Huu ni uamuzi muhimu zaidi kuliko hata madai ya kupunguza ruzuku kwa wakulima wa nchi za viwanda. Kwa upande mwingine hii ni ishara kwamba, soko huria lina manufaa kwa watu wote."
Kwa kumalizia udondozi wa magezeti ya Ujerumani leo hii, tuangalie maoni ya gazeti la HANDELSBLATT kuhusu soko huria:
"Soko huria ni zuri. Soko huria ni mfumo rahisi kabisa: Serikali zinatakiwa kufungua tu masoko ya ndani. Zinatakiwa pia kufuta ruzuku. Kwa kufanya hivyo, bei za bidhaa hushuka, na hivyo wanunuzi wa bidhaa wanaweza kununua vitu vingi zaidi. Shirika la biashara duniani linasisitiza mfumo huu. Hata hivyo baadhi ya wanasiasa hawataki kuelewa jambo hili.
Hivi sasa Umoja wa Ulaya umefanikiwa kufungua masoko yake kwa dunia nzima. Aidha hii ndiyo ilikuwa ahadi ya viongozi wa Ulaya kwenye mkutano wa Geneva. Kwa upande mwingine uamuzi huu utachapulisha pia mazungumzo yanayoendelea kwenye shirika la biashara duniani."