Udondozi wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tarehe 25.05.06
26 Mei 2006Jumanne iliyopitia katika mji mkuu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, watu 32 walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kupanga mapinduzi ya serikali.
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:
„Miezi miwili tu kabla ya uchaguzi mkuu, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inadai imetengua jaribio la mageuzi lililokuwa limepangwa na askari mamluki 32 kutoka nchi za nje.
Siku ya Jumatano iliyopita msemaji wa serikali alisema, miongoni mwa watuhumiwa hao ni Wamarekani (3), Waafrika-Kusini (16) na Wanigeria.
Aliendelea kwa kusema; lengo la watu hao ambao ni wafanyakazi wa kampuni binafsi la ulinzi lilikuwa bila shaka kuipindua serikali ya mpito na kuvuruga uchaguzi mkuu. Katika nyumba zao, taasisi za usalama zimekuta vidhibiti mbalimbali vinavyothibitisha njama hii ya kutaka kuipindua serikali ya mpito.
Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa umethibitisha habari za kukamatwa kwa raia wake watatu ambao kwa maelezo yake walikuwa kwenye safari zao binafsi. Waafrika-Kusini 16 ni wafanyakazi wa kampuni binafsi la ulinzi OMEGA SECURITY SOLUTIONS, kampuni ambalo lina mkataba wa wizara ya mambo ya ndani wa kutoa mafunzo kwa walinzi nchini humo.
Baadhi ya watuhumiwa hao walikuwa wafanyakazi wa mgombea urais anayeishi Marekani, Oscar Kashala. Huyu ni mmojawapo tu kati ya wagombea 32 wa kiti cha urais kwenye uchaguzi ujao, kiti ambacho kinagombewa pia na rais wa sasa Joseph Kabila.
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, wakati akihojiwa na jarida la FOCS, amefafanua madhumuni ya Ujerumani kushiriki kwenye ulinzi wa uchaguzi mkuu nchini Kongo-Kinshasa.
Alisema, idadi kamili ya wanajeshi wa Ujerumani watakaoshiriki kwenye zoezi hilo itategemea mipangilio ya kijeshi itakayokamilika Jumatatu ijayo. Baadhi ya askari wa Ujerumani ambao wamechukua jukumu la usafi na udhibiti wa afya kwa askari wa wote wa Umoja wa Ulaya, watapelekwa kwenye mji mkuu Kinshasa. Sehemu kubwa ya askari wa Ujerumani watapelekwa kwenye nchi ya jirabi Gabun.
Zaidi ya kukisaidia kikosi cha ulinzi wa amani cha Umoja wa Mataifa, kusimamia uchaguzi na kulinda uwanja wa ndege, bwana Jung alisema, Ujerumani inashiriki kwenye ujumbe huu kulinda pia maslaha ya Ujerumani na Ulaya.
Aliendelea kwa kufafanua kuwa, Afrika ni kontinenti la jirani, kwa hiyo utulivu na usalama wake ni muhimu kwa Ujerumani pia. Lakini akagusia pia kuwa, pamoja na wakazi wengi wa Kongo-Kinshasa kuwa maskini, nchi hii ni mojawapo ya nchi tajiri kabisa duniani.
Jarida la FOCUS limemalizia kwa kuandika: Kwa mantiki hii, nchi za Umoja wa Ulaya licha ya kwenda kusimamia uchaguzi, kuna utashi pia wa kutaka kunufaika pia na ustawi wa uchumi wa nchi tajiri, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
Lakini kinyume na mtazamo huo, wimbi la vijana wa kiafrika wanaojaribu kuingia Ulaya magharibi kwa kupitia njia za hatari kabisa, ndiyo kwanza linazidi kupamba moto. Jarida la DER SPIEGEL limeendelea kwa kuandika:
„Baada ya wakimbizi wa kughushi wa Afrika walio na fikra potofu ya kuwa na maisha bora zaidi Ulaya, kubanwa zaidi nchini Morroco, sasa wamegungua njia nyingine ya hatari zaidi: Sasa wanajaribu kuingia Hispania kupitia kwenye visiwa vya Canary, wakitokea nchi ya mbali zaidi Mauritania.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wakimbizi wa hali ya kiuchumi 6,100 wamekamatwa kwenye visiwa vya Canary; kati yao 1,500 wamekamatwa katika kipindi cha wiki mbili tu zilizopita. Tangu mwisho wa mwaka uliopita, zaidi ya watu 1,000 wamezama baharini.“
Kwa maelezo hayo yaliyoandikwa kwenye gazeti la TAGESZEITUNG ndiyo tunahitimisha udondozi wa „Afrika katika magazeti ya Ujerumani“.