Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani
4 Septemba 2006Sababu ni mkutano uliofanywa mwishoni mwa juma kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan na rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad mjini Teheran.Mada nyingine ni kashfa mpya katika jimbo la Bayern kusini mwa Ujerumani kuhusika na nyama iliyoharibika.
Kuhusu Iran,gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linasema:
Serikali ya Iran imemuhakikishia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa Teheran itashirikiana na itauunga mkono umoja huo nchini Lebanon.Hivyo Teheran imejionyesha kuwa ni mwanachama anaewajibika katika familia ya kimataifa.Annan, alitumia busara alipofanya ziara yake mjini Teheran.Kukataa kwa Marekani kuzungumza ana kwa ana na serikali ya Iran ni kosa kama Israel inavyokataa kuzungumza na Hezbollah wa Lebanon na Wapalestina wa Hamas.Mazungumzo na majadiliano tu ndio yataweza kuleta suluhisho jipya kwa Iran na amani katika Mashariki ya Kati.
Kwa maoni ya NORDWEST ZEITUNG kutoka Oldenburg, itakuwa kitisho kikubwa ikiwa Iran itakuwa na nguvu za kinyuklia:
Gazeti hilo linasema pindi Iran itafanikiwa kumiliki bomu la kinyuklia,basi hali ya kisiasa duniani itabadilika sana.Si Israel tu,ambayo kwa matamshi ya Rais Ahmedinejad binafsi,anataka kuiondoa kwenye ramani,bali hata Uturuki na sehemu za Ulaya zitakabiliwa na tishio la moja kwa moja kwani uwezo wa makombora ya masafa marefu ya Iran kwenda mbali zaidi umeongezwa. Mashindano ya kujipatia silaha za kinyuklia katika Mashariki ya Kati ni suala la wakati tu.Ye yote atakaekubali kuona Iran ikiendelea na harakati zake,basi huyo kesho atashuhudia janga ambalo hadi hivi sasa halijawahi kutokea.
Mwandishi wa habari wa NEUEN DEUTSCHLAND kutoka Berlin anaamini kuwa Marekani inataka kuzuia hilo kwa nguvu.Yeye anasema:
Kile kitakachotokea baada ya kumalizika uvamizi wa Irak,hakuna anaejua katika Ikulu ya Marekani, wizara ya mambo ya kigeni au wizara ya ulinzi Pentagon.Ni dhahiri kuwa hakuna anaekiri hilo.Kwani kuna matayarisho ya “Ujumbe wa Iran”.
Sasa hebu tugeukie mada nyingine.Baada ya kutokea tena hivi karibuni kashfa ya nyama iliyooza katika jimbo la Bayern kusini mwa Ujerumani,kwa mara nyingine tena umezuka mdahalo vipi matukio kama hayo yataweza kuzuiliwa katika siku zijazo.
Gazeti la ABENDZEITUNG kutoka Munich linatoa lawama kwa wanasiasa wanaoshughulika na mzozo huo.Linasema:
“Badala ya kuwaeleza wanunuzi wazi wazi,maeneo yaliyochunguzwa,kuwataja hao wasambazaji na makampuni yaliogunduliwa kuhusika na kashfa ya nyama iliyoharibika,waziri wa haki za wanunuzi wa Ujerumani na waziri wa afya wa jimbo la Bayern wanalaumiana.
Kwa maoni ya BERLINER ZEITUNG sababu moja kuu ya kuendelea kashfa ya nyama iliyoharibika ni kwamba ukaguzi wa viwanda vinavyohusika na nyama upo katika mikono ya serikali za majimbo.Serikali hizo hutambua kuwa makampuni hayo yanachangia kiuchumi na hivyo ihakikishwe kuwa uchumi wa makampuni hayo usidhurike kwa ukaguzi mkali.Kwa sababu hiyo daima kuna uhaba wa wakaguzi.Ikiwa ugawaji wa mamlaka utabakia na makosa hayo,basi kwa hakika kashfa nyingine ya nyama iliyoharibika ipo njiani,lamalizia Berliner Zeitung.