UCHAMBUZI WA MAGAZETI YA UJERUMANI
7 Septemba 2005
Jumatano hii,maripota wa magazeti ya Kijerumani wamejishughulisha hasa na mkutano uliofanywa kati ya mgombea ukansela wa chama cha CDU Bibi Angela Merkel na Umoja wa vyama vya wafanyakazi-DGB.Suala jingine lililotupiwa jicho vile vile ni lawama zilizotolewa dhidi ya Bush kuhusika na mpango wake wa kupeleka misaada katika maeneo yalioteketezwa na kimbunga Katrina nchini Marekani.
Tutaanzia huku Ujerumani,ambako chama cha CDU na Umoja wa vyama vya wafanyakzi bado havijaweza kuafikiana.Hata ziara ya Bibi Merkel katika makao ya DGB haikuweza kuibadilisha hali hiyo,kama gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG lilivyoripoti:
„Hadi hivi sasa vyama vya wafanyakazi vya Ujerumani havijui ni njia gani ifuatwe kuhusika na mgombea ukansela Bibi Angela Merkel.Baadhi ya wawakilishi wa wafanyakazi wangependa kwa njia ya majadiliano na Merkel,wayadhibiti mabadiliko yaliotokea katika soko huria na kuwaathiri waajiri na waajiriwa.Kwa wakati huo huo vibaba vingine vyenye itikadi kali katika vyama vya wafanya kazi vinakosoa siasa za Bibi Merkel kuhusu jamii.Vibaba hivyo vinakwenda hata umbali wa kutishia kuwa pindi kutakuwepo serikali mpya ya muungano kati ya chama cha CDU cha Merkel na cha FDP,kutakuwepo vurugu.
Lakini gazeti la Berlin TAZ linasema,mkutano wa Merkel una umuhimu wa kisiasa kwa vyama vya wafanyakazi.Linasema,“Wakati ambapo kuna uwezekano labda kwa kansela wa hivi sasa Gerhard Schroeder kuondoka kwenye uwanja wa kisiasa wa Ujerumani baada ya wiki mbili zijazo,mwenyekiti wa Umoja wa vyama vya wafanyakazi Michael Sommer ndio atakabiliwa na kipindi kigumu kabisa cha uongozi wake.Kwani atakapokutana na Merkel atapaswa kutambua kuwa pindi Merkel atakuwa kansela basi hatofanya mageuzi madogo tu kuhusu haki za wafanyakazi,suala lililo tete kwa wafanyakazi.
Na gazeti la OSTSEE ZEITUNG kutoka Rostock kwa upande wake limetaja sababu za kutokuwepo maafikiano kati ya Merkel na vyama vya wafanyakazi.
Linasema,“Merkel anataraji kubadilisha sheria zinazohusika na mishahara,kurahisisha sheria za kuwafukuza kazi waajiriwa wapya na kupunguza sauti za wajumbe wa wafanyakazi…yaani hayo ni mambo yaliopendekezwa muda mrefu na waajiri.Ni shida kuamini kuwa kweli Merkel anataka nafasi zaidi za kazi.
Na sasa tubadili mada:Gazeti la BERLINER ZEITUNG limezingatia janga la kimbunga Katrina kilichopiga kusini mwa Marekani.Kufuatia lawama za mara kwa mara kuwa serikali ilichelewa kuchukua hatua,sasa rais George W.Bush amesema yeye binafsi ataongoza uchunguzi rasmi kujua kwa nini misaada ilichelewa kufika katika maeneo ya maafa.BERLINER ZEITUNG likiandika kuhusu kashfa hiyo linasema:
„Miaka minne baada ya kutokea hujuma mbaya kabisa ya kigaidi katika historia ya Marekani,miaka minne baada ya kuzungumzwa haja ya kuwa na mpango wa kushughulikia nyakati za dharura,wakuu bado hawana hata uwezo wa kuhakikisha kuwa kuna njia ya kuwasiliana wakati kama huo.Miaka minne baada ya watu kuonywa dhidi ya mashambulio ya gesi ya sumu na kuambiwa kuwa nchi inalindwa dhidi ya mashambulio ya kigaidi,hakuna hata anaeweza kuhakikisha kwamba madaktari waliopo katika maeneo ya maafa wana uwezo wa kuwasiliana na polisi.Watu walifariki,kwa sababu timu za waokozi zililazimika kuongojea muda mrefu kabla ya kuweza kwenda katika sehemu zilizohitaji misaada.Ni dosari kubwa kwa serikali,lakini zaidi ni kwa Rais Bush.
Hata gazeti la TAGESSPIEGEL limemtupia rais Bush lawama ya kuporomoka kwa utaratibu wa kushughulikia majanga.Limesema:
„Ni mtu wa aina gani!likimaanisha Rais Bush.Na linaeleza hivi:“George Bush alitoa umuhimu zaidi kwa karamu ya chakula cha usiku pamoja na wafanya biashara mjini San Diego.Alipendelea kupiga gitaa shambani kwake.Aliona bora kuwa na mapumziko yake.Alitulia tuli,wakati wa janga la mafuriko hayo.Hatimae alijitokeza katika eneo la mafuriko kujionea mwenyewe hali ya mambo,ambayo wengine zamani walikwishaitambua ilivyo.Kwa maneno mengine alikwenda kuona kile kisichokuwepo tena,kwani hakwenda mapema na kutumia moja kwa moja mamlaka yake kwa manufaa na kutoa msaada bila ya kujali mipaka ya vyama.Alipaswa kwenda mapema zaidi.Alipaswa kuzungumza vingine, kupitisha uamuzi,kuongoza na kuwapa matumaini walioathirika.Alau angebakia nao“ laeleza TAGESSPIEGEL.