uchambuzi wa magazeti ya ujerumani leo.
22 Juni 2004Katika maoni ya wahariri wa magazeti leo, suala la kitovu ni hotuba ya mwenyekiti wa chama kinachotawala nchini Ujerumani bwana Franz Münterfering,yenye lengo la kugusa mioyi na fikara za wanachama wa chama hicho baada ya matokeo mabaya ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.
Juu ya hotuba hiyo gazeti la Frankfurter Rundschau linasema kwamba msimamo wa mwenyekiti Münterfering sasa umeonekana bayana miongoni mwa wanachama wengine. Gazeti linatilia maani kauli ya bwana Münterfering kwamba chama chake cha Social democratic Party kinachotawala hapa nchini siku zote kitahitajika na kwamba chama hicho hakina haja ya kuwa cha upinzani kwani upinzani unaleta madhara kwa nchi.Hatahivyo mhariri anasema kuwa chama cha SPD chenyewe kimo katika hali ya kuvunjika moyo.
Gazeti linalotolewa katika mji wa Cologne Tageszeitung linasema kwamba chama cha bwama Münterfering sasa kimekwama.
Mhariri anauliza sasa chama hicho kitafanya nini,? Jee kitafanya kichwa ngumu na kusonga mbele ama kitabadili msimamo juu ya programu yake ya mageuzi?
Likitoa maoni yake juu ya hali inayoikabili chama cha SPD gazeti la Handelsblatt linaeleza kuwa kimsingi chama hicho hakiwezi kufanya mabadiliko kisiasa bali ni katika muundo tu. Mhariri anasema kuwa hamna maudhui katika ujumbe unaotoka katika chama hicho. Mhariri anatilia maanani kwamba yanayosikika ni mambo ya yale yale ya tokea miaka nenda rudi katika programu za chama,kwamba matajiri watozwe kodi zaidi kwa manufaa ya wananchi na makampuni pia yalipe kodi za juu. Mhariri anaandika kuwa vidokezo kama hivyo vinaweza kuwa vya kuvutia kwa wanachama wenye mlengo wa kisoshalisti katika chama hicho,lakini iwapo mtu anazingatia hali halisi, atatambua kwamba kisiasa mipango hiyo haitaleta mavuno asilani. Likitoa hoja katika mantiki hayo hayo,gazeti lingine Mannheimer Morgen linakumbusha vidokezo juu ya :mishahara ya kima cha chini kwa wote,juu ya kodi ya msingi kwa makampuni na juu ya kutoza kodi mali ya urithi. Mhariri anaeleza ushukivu ,iwapo kwa programu kama hizo itawezekana kwa chama cha Social Democratic Party kurejesha tena imani miongoni mwa watu wasiokuwa na ajira,wastaafu na watu wenye kipato cha chini hapa nchini. Gazeti la Neues Deutschland linauliza swali la kimsingi juu ya kauli ya mwenyekiti wa chama cha SPD bwana Münterfering kwamba chama chake kitaendelea kuhitajika. Gazeti linauliza jee kuna sababu gani kwa chama hicho kuhitajika? Na gazeti linalotolewa katika mji wa Chemnitz mashariki mwa Ujerumani linasema kuwa chama cha Social Democratic Party kimo katika hali ya kupigania uhai wake. Gazerti hilo Freie Presse linaeleza kwamba chama hicho sasa kinakabiliwa na hofu kiasi kwamba hakijitambui, lakini hiyo ni hali halisi. Ostsee Zeitung linasema kwamba mwenyekiti wa chama cha SPD anajaribu kuwapoza wanachama wengine lakini hana dawa nyingine licha ya kutumia silika juu ya mamlaka ya uongoz kwa kusema kuwa chama chake kinataka kuendelea kutawala na siyo kugeuka chama cha " upinzani" Ushauri mzuri unatoka kwa mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten anayesema kwamba chama SPD sasa kimo katika hatua ya mabadiliko,lakini bwana Münterfering hakika siyo mtu atakayefaa kuleta mabadiliko hayo.
Tunamaliza kw maoni ya gazeti la Frankfurter Allgemeine linalosema kwamba chama cha Social democratic Party sasa kinajitesa baada ya kuzinduka kutoka kwenye mshtuko kufuatia matoke ya uchaguzi.Chama hicho kimo katika hali ya kukata tamaa mhariri wa gazeti anaeleza kama mwenyekiti wake anavyoonyesha Mhariri anaeleza kuwa kinachoweza kutumainiwa kutoka kwa mwenyekiti huyo ni miujiza..