Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
28 Juni 2004Kuhusu kuteuliwa waziri mkuu wa Ureno Jose´Manuel Durao Barosso kushikilia wadhifa wa rais mpya wa umoja wa ulaya mjini Brussels, gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKRFURTER RUNDSCHAU, linaandika: Kuna sababu mbali mbali zilizopelekea kuteuliwa kwake, kwanza, kwa sababu ni kiongozi wa serikali nchini mwake Ureno, pili kwa sababu anatoka kambhi ya wakonsavativ, na tatu kwa sababu haelemei upande wowote katika umoja wa ulaya. Mteule Barosso anavutia masilahi ya wengi katika umoja huu, ijapokuwa hakuwahi kushikia usukani shuguli za nchi za ulaya kwa jumla.
Kuhusu mada hii gazeti la mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Potsdam, MÄRKISCHEN ALLGEMEINE, linauliza kwanza: je, ni nani aliyekuwa akijua jina la waziri-mkuu huyu wa Ureno hadi ijumaa iliyopita? Ijapokuwa hayo Jose´Manuel Durao Barosso asitazamwe kama ni mteule wa dharura kama rais mpya wa halmashauri ya umoja wa ulaya. Amefanikiwa kuteuliwa hasa kwa sababu hakupatikana mgombea mwingine mwenye kipaji cha uongozi wa shuguli za nchi za ulaya kwa jumla na maarifa ya kutosha ya siasa za kimataifa, ambaye angeweza kuungwa mkono na serikali za nchi zote zilizo wanachama.
Gazeti la shuguli za biashara HANDELSBLATT, linatukamilishia mada hii kwa kuandika: Mteule Barosso si mashuhuri sana kisiasa hata nchini mwake Ureno. Ikumbukwe tu jinsi alivyoshindwa wakati wa uchaguzti wa bunge la ulaya mjini Lisbon. Kuteuliwa kwake kunawashangaza wengi pia kwa sababu hakuwahi kuwa mashuhuri katika majukwaa ya umoja wa ulaya, ijapokuwa alikuwa mwenyyeji wa mkutano wa kilele muda mfupi kabla ya kuanza vita vya Irak.
Gazeti lingine la kusini mwa Ujerumani STUTTGARTER ZEITUNG, linajishugulisha na mada nyingine kabisa, nayo ni mjadala unaoendelea hapa nchini Ujerumani, juu ya kurefushwa muda wa kufanya kazi kuwa ni masaa 40 kila wiki, linatoa maoni: Yale ambayo waajiriwa walifanikiwa kupata kwenye migomo ya zaidi ya mwongo mzima, ya kufanya kazi kwa muda wa masaa 35 kwa wiki yanaelelekea yalikuwa bure. Kwani baadhi ya mikoa ikishikiwa usukani na Bavaria, inashikilia ufanyaji kazi kwa muda wa masaa kati ya 40 na 42. Ndio maana chama cha watumishi wa huduma za kijamii VERDI, kiko mbioni kupinga madai ya mikoa hiyo, hata kabla ya kufanyika duru ya kujadili masharti ya kazi na mishahara mwishoni mwa mwaka huu. Inaelekea waajiriwa wengi wako tayarai kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi, iwapo tu nafasi zao za kazi haitahatarishwa.
Gazeti la HESSISCHE/ NIEDERSÄCHSISCHE ALLGEMEINE, linachangia mada hii kwa kuandika: Ufanyaji kazi kwa muda wa masaa 40 kwa wiki, si swala la jinsi viongozi wanavyoweza kuaminiwa. Kwa madai yao wanaonyesha jinsi wanavyoshindwa kupitisha maamuzi ya busara katika mashindano ya kimataifa. Mfano mwema ni ule wa viongozi wa shirika mashuhuri la kiuchumi la Siemens walivyo na kipaji cha kupitisha maamuzi yanayohusika.
Tunakamilishia uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama maoni ya gazeti la mji wa Munich, ABENDZEITUNG, linapoandika kuhusu mada hii: Mashirika mengi katika Ujerumani wakati huu yanajikuta katika mzozo kwa sababu bidhaa zao ni ghali sana katika masoko duniani. Yanafungua matawi mapya katika nchi za nje, kwa sababu kuongeza muda wa kufanya kazi,
hapa nchini kunamaanisha yanaweza kuuza bidhaa zao kwa bei nafuu zaidi. Swala hili la kuongezwa muda wa kufanya kazi ni chungu kwa waajiriwa wengi, lakini ni wazo linalochangia jitihada ya kupunguza ukosefu wa ajira kwa jumla.