Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
29 Juni 2004Gazeti mashuhuri la Berlin NEUS DEUTSCHLAND, kuhudu kukabidhiwa mamlaka serikali mpya ya mpito nchini Irak, linaandika: Kwa hatua hii rais wa Marekani George W.Bush, ameweka jiwe la msingi la kuleta mabadiliko nchini Irak. Ametumia akili kuifanya sherehe hiyo ya siri kabisa na isiyo hudhuriwa na watu wengi, hasa kwa sababu za usalama. Lakini hatua hii ya kukabidhiwa mamlaka serikali ya mpito, hakumaanishi kupatikana hali shwari nchini Irak wakati ujao, wala dira ya siasa za Marekani nchini humo. Sababu ni kwa kuwa hofu na matumizi ya nguvu yanaendelea kutawala kila kukicha nchini humo, ambayo sura yake imeteketezwa kwa sehemu kubwa. Cha kusikitisha ni ukweli kwamba, hakuna dalili za uwezekano wa kuchuzkuliwa hatua za kuijenga upya nchi hiyo mnamo siku za usoni. Hii ni hatua ambayo haiwahakikishii WaIrak wengi matumaini ya kujitegemea, kama wanavyoahidiwa na serikali ya mpito ya Bagdad pamoja na serikali ya Washington. Sababu ni kwa kuwa, mamlaka ya kijeshi na kiuchumi, yatakabia kwanza mikononi mwa wakaliaji.
Nalo gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU, kuhusu mada hii linaandika: Matatizo yanayoikumba Irak, yanaweza kutatuliwa na WaIrak wenyewe tu, ndio maana wanahitaji mamlaka ya kujitegemea. Sio matumaini ya karatasini pekee, bali pia katika maisha ya kila siku. Na hayo yanawezekana tu kwa Irak kuungwa mkono na misaada ya kimataifa. Lakini endapo Marekani, Uingereza pamoja na wasshirika wao, zitaendelea kuwa ndizo mabwana, hapana shaka matumaini yote ya mustakabali wa Irak yatakuwa bure. Ushirikiano kati ya serikali ya mpito na watawala wa kijeshi usingechangia chochote jitihada ya kuhifadhi amani nchini Irak.
Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT, linasisitiza: Ujitegemeo unamaanisha nchini humo ni nani aliye na uwezo wa kusimamia hali ya hatari. Hayo yanawezekana tu, iwapo serikali mpya ya mpito, ingefuata mkakati wa kuyaoanisha makundi yote yanayohusika ya kitaifa, yale ya wasuni, wafuasi wa chama-tawala cha zamani cha Baath, ya wale wanaofanya maasi ya kulihangaisha taifa na mengineyo.
Nalo gazeti lingine mashuhuri la kusini mwa Ujewrumani SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linazingatia mada nyingine kabisa, nayo ni mvutano unaoendelea hapa Ujerumani kati ya chama-tawala cha Kansela SPD na shirika la vyama vya wafanya kazi DGB, kuhusiana na mpango wa mageuzi wa serikali – linaandika:
Kiongozi wa wabunge wa chama cha upinzani CDU, Friedrich Merz pamoja na mwenyekiti wa chama kingine cha upinzani cha FDP, Guido Westerwelle, wanatazama tu kwa furaha jinsi kambi mbili za SPD na DGB, zinavyovutana.Waidhinishaji hawa wawili wa masoko ya kiliberali, hawana hofu kuhusu mpango wa mageuzi wa Kansela Schröder wala hatima ambayo huenda ingekikumba chama chake SPD. Kile mabwana Merz na Westerwelle wanadhamiria, ni kulifanya kuwa hata pana zaidi pengo kati ya sehemu ya wanachama wa SPD na ya shirika la vyama vya wafanya kazi.
Mwenyekiti wa chama cha FDP, Westerwelle, hata anakwenda umbali wa kumtaja mwenyekiti wa chama cha watumishi wa huduma za kijamii VERDI, Bsirski, ni mhaini wa jitihada ya kutatuliwa tatizo la kuzidi kupanda idadi ya wasio na ajira katika Ujerumani. Mwisho wa uchambuzi wa magazetzi ya Ujerumani hii leo.