Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
1 Julai 2004Kuhusu mada hii ya sherehe za kuagwa rais wa zamani Johannes Rau na kuapishwa rais mpya mfuasi wake Horst Köhler, gazeti mashuhuri la hapa mjini Bonn GENERAL ANZEIGER; linaandika: Baada ya rais mtangulizi Johannes Rau sasa Ujerumani pia imebahatika kupata rais mpya mwenye kipaji cha uongozi. Hii leo rais mpya aliapishwa katika sherehe ambapo rais wa zamani alisema anafurahi kumkabidhi wadhifa wake mfuasi wake. Ana maoni kwamba, raia wa Ujerumani wana sababu za kumfurahia rais wao mpya, ambaye kwa muda wa nusu mwaka tayari amekuwa akiwashugulikia awezavyo, hasa kwa sababu hakusahau kuwa ni mmojawapo miongoni mwao.
Gazeti la NÜRNBERG NACHRICHTEN, linachangia mada hii linapoandika: Kama walivyokuwa watangulizi wake, Heuss, Heinemann, von Weizsäcker na Herzog, rais wa hadi sasa Johannes Rau alithibitisha kipaji cha kuwa mwakilishi wa dola, kwa mfano, alipotia saini sheria mbali mbali za dola, kuwaapisha mawaziri wapya au hata kuwapatia hati wale wanasiasa walioagwa.
Johannes Rau alikuwa ni rais mwenye kushikilia mkondo wa kisiasa, na alikuwa ni rais mmojawapo aambaye kutokana na maarifa yake alitambua nini inamaanisha kuzaliwa katika enzi ya manazi katika Ujerumani. Kama walivyokuwa marais watangulizi wake, alijua barabara jinsi wajerumani walivyojifunza namna ya kuishi kwa machungu ya enzi hiyo.
Nalo gazeti la RHEIN-ZEITUNG lina haya ya kuongezea kuhusu mada hii:
Wakati wa kuapishwa rais mpya, na mwenyekiti wa zamani wa shirika la fedha la kimataifa, Horst Köhler, hapana shaka Ujerumani imebahatika kwa sababu ya kujikuta sasa katika kuipindi cha mageuzi makubwa. Ndio maana hakuna mtangulizi wake mwingine, aliyekabiliwa na majukumu muhimu ya dola kuliko rais mpya Horst Köhler.
Nalo gazeti mashuhuri la Berlin TAGESSPIEGEL, linajishugulisha na kule kukabidhiwa dikteta wa zamani wa Irak Saddam Hussein mahakhama maalum mjini Bagdad, kwa kuandika: Kesi dhidi yake, ambayo itafunguliwa baada ya miezi michache ijhayo, inafanana na mtihani kama Irak mpya ni dola lenye kufuata misingi ya haki. Na hapana shaka matangazo ya televisheni kutoka mahakhama hiyo, yatakuwa ya kuvutia wengi kote ndani na nje ya nchi hiyo. Naam, Saddam Hussein anafikishwa mahakhamani kwa sababu ya vitendo alivyofanya vya kikatili, lakini usisahauliwe ukatili unaofanywa na wenzi wake katika badhi ya nchi za kiarabu.
Gazeti mashuhuri la mashariki mwa Ujerumani MÄRKISCHE ODER-ZEITUNG, kuhusu mada hii linaandika: Ingekuwa bora iwapo Saddam Hussein angefanyiwa kesi katika mahakama ya kimataifa, lakini wamerikani walikataa. Kwa sababu ya sura ya sasa ya machafuko na matumizi ya nguvu nchini Irak, isingewezekana kumfanyia kesi katika mahakhama hiyo ya kimataifa. Hii ni kesi ya kihistoria ya ulipizaji kisasai.
Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti Lingine la mashariki DRESDENER NEUSTEN NACHRICHTEN, kuhusu mada hii: Baada ya kuangushwa kwa mtawala huyu wa umwagaji damu Saddam, ni mahakama ya kimataifa pekee ambayo ingeweza kumfanyia kesi, kama anavyofanyiwa sasa kiongozi wa zamani wa iliyokuwa Yugoslavia Milosevic pamoja na wenzi wake. Saddam Hussein hawezi kutazamwa kama si mhalifu. Kwa sababu hii wengi ndani na nje ya Irak, wanasubiri kwa hamu kuona jinsi dikteta huyu wa zamani Saddam Hussei atakavyochukuliwa hatua, kwa sababu kesi yake inaambatana moja kwa moja na hisia za ulipizaji kisasi.