Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
5 Julai 2004Kuhusu uwezekano wa kuundwa chama kipya na wanachama wasioridhika wa tawi linaloelemea upande wa kushoto katika chama-tawala SPD, gazeti la kusini mwa Ujerumani HESSISCHE/ NIEDERSÄCHSISCHE ALLGEMEINE, linaandika: Kwa kweli wasocial-democrats wanajibebesha binafsi mzigo mzito kwa mpango wao wa mageuzi ya huduma za kijamii Agenda 2010. Wanachama hao wanaopanga kuunda chama kipya, ni wale ambao wanahisi mpango huo wa serikali hautilii uzito kutosha haki za kijamii. Ndio maana haistaajabishi kwamba wanachama wa kawaida wanahisi kukatishwa tamaa na kuhamakishwa. Nia ya kuundwa chama hicho kipya, ni kuwatuliza wanachama hao ambao hawaridhiki, hasa kwa sababu chama-tawala SPD, kinatoa ahadi nyingi, ambazo hakitekelezi.
Kuhusu mada hii gazeti la mji mkuu BERLINER ZEITUNG, linaandika: Kansela Schröder, mwenyekiti wa chama Münterfering pamoja na viongozi wengine chamani, inaelekea hawahangaishwi sana na nia ya wanachama hao wa jadi ya kutaka kujitenga na kuunda chama kipya baadaye mwaka huu. Sababu ni kwa kuwa, hadi sasa zinasikika fununu tu bila kutanjwa hata majina ya wanachama wa safu ya pili au ya tatu katika siasa. Kuna haja ya viongozi wa SPD kuwa macho, kwa sababu nia hiyo ya kuundwa chama kipya, inaungwa mkono nyuma ya pazia na vyama vya wafanya kazi.
Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE, linasema sababu mojawapo ya wanachama hao kutoridhika, ni kwa kuwa ustawi wa uchumi unakwama tangu karibu miaka minne sasa, na zaidi ya hayo vyama vikubwa vya umma vya kisiasa, havina imani tena na mpango huo wa mageuzi wa serikali. Ndio maana kuna wanasiasa wengi, wanaokaribisha wazo la kuchimbwa msingi mpya wa busara kwa kuundwa chama kipya cha mrengo wa kushoto. Lakini inaelekea mradi huu hautafanikiwa kwa sababu hoja za kupinga tu siasa za mageuzi pindi kujitenga na kuunda chama kipya, haziwezi kuaminika.
Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN, linachangia mada hii kwa kuandika: Wakati huu Kansela anabinywa kutoka kila upande. Wakati upande wa vyama vya upinzani unaposema, mpango wa mageuzi wa serikali hauendi mbali kutosha, nao upande wa vyama vya wafanya kazi unakosoa kwamba, mpango huo wa Agenda 2010, hautilii maanani maswala muhimu ya mnaisha ya kijamii, na unawakatisha tamaa tu wapigaji kura wa jadi wa SPD. Si ajabu basi kwamba baadhi ya wanachama hawaridhiki na wanataka kukipa kisogo SPD. Na kama hazitachukuliwa hatua za kuridhisha wanachama hao wa mrengo wa kushoto, hapana shaka ugomvi na mvutano huu utaendelea.
Gazeti la LANDESZEITUNG LÜNEBURG, nalo linasema: Yaliyomo ndani ya mpango huo wa mageuzi wa serikali, hayawezi kuachwa kama yalivyo, iwapo nia yake ni kuchangia jitihada ya kuwahakikishia wananchi maisha ya neema wakati ujao, yaani haki sawa kwa kila raia katika jamii. Lakini kwa bahati mbaya, cha pekee kinachosikika mara nyingi katika Ujerumani ni manungúniko pekee ya wale wanaoonea wivu maisha ya neema ya raia wenzi wao katika nchi nyingine za viwanda.
Tunakamilisha uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la kusini mwa Ujerumani SÜDDEUTSCHE ZEITUNG kuhusu siasa za ndani linaposhikilia: Siasa hizi za mageuzi zinawahangaisha wengi katika jamii. Kitu muhimu kukumbukwa ni kwamba, yule aliye na ajira, anabidi kufanya kazi muda mrefu zaidi na kuacha dai la kupatiwa mapumziko maalum ya wiki moja. Na wale raia wasio na ajira, wanakabiliwa na tatizo kubwa la kupunguzwa misaada ya kifedha ya serikali na kuandamwa na maofisa wa serikali katika makazi yao. Raia wanahisi kukatishwa tamaa hasa kwa sababu, viongozi wa vyama vya kisiasa, vyama vya wafanya kazi na waajiri, badala ya kuketi kwenye meza moja na kulitafutia utatuzi swala hili la mageuzi, wanaendelea tu na mtindo wao wa kawaida wa kuvutana.