Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
22 Septemba 2004Ijapokuwa kuna uwezekano wa wanasiasa na wanauchumi wa Ujerumani kuafikiana mapatano kuhusu mafunzo ya kazi, ambayo huenda yakaanza kuwa na nguvu kuanzia tarehe 30 septemba, maalfu ya vijana wa Ujeumani wataendeelea kuishi bila ya maelekeo yoyote ya kupata nafasi ya kajifunza kazi yoyote. Kuhusu mada hii gazeti mashuhuri la hapa jijini Bonn, GENERAL ANZEIGER, linaandika: Inaelekea kuna uhusiano wa karibu kati ya mafanikio ya karibuni ya vyama vya mrengo wa kulia ya kuingia katika mabunge ya mikoa miwili ya mashariki mwa Ujerumani baada ya chaguzi za karibuni na haja ya kuwahakikishia vijana nafasi za elimu ya kazi. Iwapo vijana hawana maelekeo yoyote kuhusu mustakabali wao, huwa hawana chingine cha kufanya ila kuupa kisogo mfumo mzima wa kisiasa wa dola. Hii ndiyo sababu kwanini jitihada ya upatanishi kati ya wanasiasa na wanauchumi ni muhimu sana katika maisha ya kijamii. Vijana wasiingiwe kamwe na hisia kama dola linaacha mkono masilahi yao.
Gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani SÜDDETSCHE ZEITUNG, linachangia mada hii kwa kuandika: Hata ikiwa mapatano haya hayatachangia kuziba pengo lililopo, alao yanatilia maanani thamani ya kumhakikishia kijana nafasi ya kujielimisha ajira inayomkaa moyoni. Hata serikali inajaribu kwa mpango wake wa mageuzi katika masoko ya ajira, kuhakikisha kwamba, mara kijana akishamaliza shule, asigeuke kamwe ni mhanga mmojawapo wa wale wanaokosa nafasi za ajira. Kuna haja kubwa ya wote kwa pamoja, wanasiasa kwa wanauchumi, kutembea mkono kwa mkono katika kutatua matatizo yanayowakabili vijana.
Gazeti la mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Gera OSTTHÜRINGER ZEITUNG, kuhusu mpango wa shirika la reli la Ujerumani wa kupandisha nauri za usafiri, linauliza, je, ni sababu gani ziliko nyuma ya nia hii. Linaonya: Ni nia ya hatari wakati mwenyekiti wa shirika la reli Mehdorn anapoidhinisha mpango huu kinyume cha masilahi ya viongozi wa matawi ya shirika lake. Isisahauliwe kwamba, hii ni nadharia tu kwani huenda mpango wake ukavunjikilia mbali. Tukumbushe tu utaratibu wa nauri za usafiri wa mwaka uliopita, ambao uliwashurutisha abiria wengi kuamua kuchagua usafiri wa barabara badala wa reli. Iwapo shirika la reli linataka kujikwepa na matatizo ya kiuchumi, basi inalibidi kuacha mpango huu wa kunyanyua nauri, kuhakikisha huduma bora, kuafikiana mapatano rahisi za masharti ya kazi na mishahara na kuhakikisha kwamba treni hazichelewi safarini.
Gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG kuhusu mada hii linaandika: Kwa sababu ya mpango wake haimshangazi mtu kuona jinsi mwenyekiti wa shirika la reli Mehdorn alivyopatwa na fadhaa kubwa. Hana nia ya kuzingatia mikakati ya kisiasa katika kutatua matatizo ya usafiri, bali muhimu kwake ni kuboreshwa mikakati ya kuwahudumia abiria. Kwa sababu hii mpango huu unaelekea ni chanzo cha mvutano mpya katika jamii.
Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT, kuhusu pendekezo la waziri wa ndani wa Ujerumani Otto Schily la kujengwa kambi ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi katika kaskazini mwa Afrika. Linaandika: Waziri Schilly ana mpango wa kuijulisha tume ya mashauri ya ndani wiki ijao yaliyomo kinaganaga kuhusu pendekezo lake. Lakini Die Welt linakumbusha jinsi Otto Schily hakupendezwa sana na namna alivyokosolewa na waziri wa nje Joschka Fischer, kwamba alitangaza pendekezo lake hadharani kabla ya kuchunguzwa kisiasa umuhimu au athari zake.