Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
27 Septemba 2004Gazeti la STUTTGATER NACHERICHTEN, kuhusu matokeo ya uchaguzi wa mabaraza ya miji na vijiji uliofanyika jana katika mkoa wa magharibi wa North-Rhein Westfalia,linauliza swsali muhimu, je, ni nani anayeweza kushamgilia ushindi, hasa ikikumbukwa kwamba, chama cha CDU katika duru ya pili kimepindukia ndicho madhubuti kabisa, ijapokuwa kimepoteza kura karibu asilimia 7 kulinganisha na uchaguzi wa mwaka 1999, na wakati chama kikubwa cha pili SPD, halikadhalika kikipoteza kura kulinganisha na matokeo ya uchaguzi miaka mitano iliyopita? Haya ni matokeo yaliyo machungu kabisa kwa SPD tangu vita vya pili vya dunia. Kinachovutia hasa ni hali kwamba, vyama vikubwa CDU na SPD, havikunufaika na malalamiko ya wapigaji kura wa vyama vidogo.
Gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT, kuhusu mada hii linaandika: Uchaguzi katika North-Rhein Westfalia, umefanyika kwa kutawaliwa na hali ya vyama vikubwa CDU na SPD kuwa na wasiwasi kama vitashinda au vitapoteza tena wapigaji kura. Wakati chama cha CDU kinapobakia ndicho madhubuti kabisa ijapokuwa kimepoteza wapigaji wengi wa jadi, nacho SPD hakina wasiwasi kwa sababu, ijapokuwa kimepoteza kidogo, kimesalia katika safu zake za kawaida.
Nalo gazeti mashuhuri la kusini mwa Ujerumani SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linachangia mada hii kwa kuandika: CDU kimepokonywa fursa ya kuwa chama cha busara kwa mamilioni ya raia kuelekea siasa za serikali. Kilichelewa sana kujitokeza kama chama cha mageu8zi ya kiutu. Lakini alao kimefuata shauri la mwenyekiti wake Angela Merkel la kufunga macho na kusonga mbele. Lakini hakiwezi kufunga macho kwani huenda kikakumbwa na kishindo kikubwa zaidi kwenye uchaguzi wa serikali ya mkoa huu wa North-Rhein Westfalia mwezi mei mwaka ujao wa 2005.
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linauliza, je nini matokeo ya uchaguzi huu wa mabaraza ya miji na vijiji yatasaidia uchaguzi wa serikali ya mkoa huu mwakani? Hayatakuwa na maana yoyote, kwani ushindi wa chama cha CDU mwaka 1999, hakupatikana kutokana na nguvu zake binafsi. Chama hiki kina bahati hasa zikikumbukwa kashfa chungu nzima za rushwa zilizokikumba majuma machache baadaye.
Mkoa wa kaskazini mwa Ujerumani wa Niedersachsen, umekosoa vikali wazo la kufanyika karibuni mkutano wa mawaziri wa utamaduni wa serikali za mikoa mada inayozingatiwa na gazeti lingina la kusini la BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linapoandika: Msimamo huo unatokana na ukweli kwamba, mikutano ya mawaziri wa mikoa yote 16 ya Ujerumani, humeza kiwango cha Euro Milioni 50 kila mwaka. Mkoa huo wa kaskazini unauliza kiwango hicho kikubwa kitumike kwa faida gani? Ili kuweza kuandaa mkutano huo mkoa huu wa Niedersachsen umeagizwa uugharamie kwa kiwango cha Euro Milioni 2 na nusu, dai ambalo halieleweki na walipaji kodi wengi.
Gazeti mashuhuri la biashara HANDELSBLATT, kuhusu mada hii linaandika: Kwa hakika mikutano hii ya kila mwaka ya mawaziri wa utamani ni mzigo mzito kwa walipaji kodi. Iwapo waziri-mkuu wa mkoa huo Christian Wulff anataka kubana matumizi inambidi kubuni mkakati mpya.
Tunakamilishia uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti mashuhuri la mji mkuu BERLINER ZEITUNG, linapoandika kuhusu mada hii: Sasa inabidi kutokea hali katika Ujerumani, ambayo tayari imeshazuka katika nchi nyingine. Nayo ni kwamba nchi hizo zimeiandalia mikoa yao mifumo kabambe ya namna ya kubana matumizi. Wakati ujao mikoa ya Ujerumani itabidi iwe ikitembea mkono kwa mkono pia katika maswala ya matumizi ya pesa.