Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
13 Oktoba 2004Kuhusu hatua iliyochukuliwa jana ya kumrejesha Uturuki kiongozi wa itikadi kali za kiislamu Metin Kaplan kutoka Ujerumani gazeti la mji wa Ludwigshafen DIE RHEINPHALZ linaandika: Kitu kimoja kinachojulikana kwa hakika ni kwamba, kiongozi huyu wa itikadi kali za kiislamu Metin Kaplan, hatakuwa tena na fursa ya kusambaza chuki zake dhidi ya wenye kufuata misimamo au dini nyingine katika Ujerumani. Kwa hatua hii ya kumrejesha nyumbani Uturuki, mahakimu wametoa ishara kwamba, hata wao pia wako gtayari kuchangia harakati za kupambana na wenye kufuata itikadi kali wa kiislamu. Ilidumu muda wa dadika 90 tu kuanzia pale alipokamatwa hadi kuruka ndege yake kuelekea Ankara.
Nalo gazeti mashuhuri la Kolon, KÖLNER STADT-ANZEIGER, kuhusu mada hii linandika: Metin Kaplan ameshaondoka na huenda ikawa hakuna mtu atakayetokwa na tone la huzuni,kwani licha ya kuwa ni mchocheaji pia alikuwa wakati huo huo ni mfuasi wa itikadi kali za kidini na za chuki.
Na kwa sababu ya mabadiliko yaliyotokea tangu karibuni nchini Uturuki, inaweza kutumainiwa tu kwamba, atafanyiwa kesi ya haki kwa kiasi fulani.
Gazeti la mji wa magharibi wa Essen WEST-DEUTASCHE ALLGEMEINE ZEITUNG, linachangia mada hii kwa kukumbusha: Tangu miaka ya karibuni Metin Kaplan amekuwa mashuhuri duniani karibu kama kiongozi mwingine mwenye kufuata itikadi kali na kiongozi wa Wakurdi Abdullah Öcalan. Wazalendo hawa wawili hapana shaka watakuwa ni mtihani mgumu kwa Uturuki, kama kwa kweli itawachukulia hatua kwa msingi wa haki, ambazo zinadaiwa kama sharti mojawapo la kimsingi la kuiwezesha Uturuki kupatiwa uwanachama katika umoja wa ulaya.
Kuhusu kujiuzulu nyadhifa zake za kisiasa kama kiongozi wa kundi la vyama-ndugu vya upinzani CDU na CSU katika bunge mjini Berlin na makamu wa mwenyekiti wa chama cha CDU, Friedrich Merz, gazeti la kusini ALLGEMEINE ZEITUNG linaandika:
Hiki ni kishindo hata ikiwa ametangaza kujiuzulu kwake wakati chama chake CDU kikabiliwa na matatizo. Kujiuzulu kwake hakutaathiri sana siasa za chama wala umashuhuri wa mwenyekiti Merkel, ambaye si mwanasiasa rahisi katika kushikia usukani shuguli za uongozi wa chama.
Gazeti mashuhuri ala Berlin NEUS DEUTSCHLAND kuhusu mada hii linaandika: Inaelekea tangazo la kujiuzulu kwa Friedrich Merz linamkaa moyoni Angela Merkel. Friedrich Merz ambaye halikadhalika ni mwenye kushikilia misimami mikani ya kisiasa, hapana shaka anaungwa mkono na wale katika Ujerumani ambao wanataka kuzingatiwa siasa mpya za kiliberali, na wale ambao hawaridhiki kwamba, chama hiki cha umma CDU, kinashikiwa usukani na mwenyekiti kutoka mikoa mipya ya mashariki mwa Ujerumani.
Mada hii inachangiwa na gazeti mashuhuiri la biashara HANDELSBLATT kwa kuandika: Huenda ikawa kwamba, Friedrich Merz kwa hatua yake atafanikiwa kujikwamua kisiasa. Endapo mgomea wadhifa wa waziri-mkuu wa mkoa wa North-Rhein-Westfalia kutoka chama cha CDU Jürgen Rüttger atashindwa
kwenye uchaguzi mwakani wa serikali ya mkoa, basi huenda ikawa mwenzi wake Merz angepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa CDU mkoani humo. Na hayo muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa shirikisho. Kwa Angela Merkel hiki kingekuwa ni kishindo kikubwa. Mwisho wa uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo.