Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
18 Oktoba 2004Kwanza tutazame yale yanayoandikwa na gazeti mashuhuri la hapa jijini Bonn BONNER GENERAL-ANZEIGER kuhusu hali ya kuhangaisha iliyozuka ndani ya chama cha upinzani CDU katika bunge mjini Berlin, linakumbusha: Tangu majuma kadhaa yaliyopita, mwenyekiti wa chama cha CDU, Angela Merkel, amekuwa akipoteza mfululizo umashuhuri wake hadharani pia kwa sababu chama chake halikadhalika kinadidimia umashuhuri wake. Kwa sababu hii wafuasi wa chama hiki wanadai kurekebishwa mafungamano ya kindugu kati yake na chama mwenzi wake cha mkoa wa Bavaria CSU. Inaelekea kama Angela Merkel anakabiliwa na hali kama ile iliyokuwa ikimkabili kwa muda mrefu kansela Gerhard Schröder. Nayo ni kushikilia mpango wa mageuzi, hata ikiwa usingefanikiwa. Endapo mpango huu hautafua dafu basi itabidi kusubiriwa hadi baada ya uchaguzi mkuu wa shirikisho wa mwaka 2006.
Gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT, nalo linajishugulisha na majukumu ya mwenyekiti wa chama Angela Merkel kwa kuandika: Mwanamke huyu kutoka mashariki, bado hajafanikiwa kama anavyotakiwa, mara hujikuta kipweke katika vikao vya chama, hasa kwa sababu anakabiliana na baadhi ya wale walio na kinyongo naye na wanaojaribu kupimana naye misuli ya hatamu. Lakini imekutikana hali katika vyama-ndugu CDU na CSU kwamba, Angela Merkel hana hisia za nini inamaanisha mwelekeo wa kikonsavativ. Na ndio maana linazuka swali baadhi ya nyakati kama kwa kweli angefaa kuwa mgombea wa wadhifa wa kansela? Ingekuwa bora iwapo swala hili lingetafutiwa ufunmbuzi hivi sasa, kwa sababu vyama-ndugu vya CDU na CSU vinabidi kusimama katika jukwaa la pamoja la mwelekeo wa kindugu. Ni kwa njia hii tu ambapo vyama hivi vinaweza kujikinga dhidi ya siasa za serikali.
Gazeti mashuhuri la mji wa magharibi wa Düsseldorf,WESTDEUTSCHE ZEITUNG, linapojihugulisha na mpango wa kulifanyia mageuzi tawi la shirika la magari General-Motors lililoko katika mji mwingine wa magharibi wa Bochum la Opel, linaandika: Hakuna mtu anayeweza kusimamia hasira na hangaiko ya wafanya kazi wa Opel mjini Bochum. Hata chama cha wafanya kazi za chuma IG-Metal, kinashindwa kupatanisha, hakuna mfanya kazi hata mmoja anayetaka kusikia hata neno moja kutoka kwa viongozi wake. Isitoshe, kampuni hili halitazamii kupata msaada wowote kutoka kwa serikali ya mkoa. Zaidi ya hayo isisahauliwe kwamba, tawi hili la maghari mjini Bochum, liliadhibiwa mwaka uliopita kwa sababu ya msimamo wa Ujerumani wa kupinga vita vya Irak, kinyume cha zile nchi ambazo ziliviunga mkono kama vile Poland. Haya ni kwa mujibu wa viongozi shirikisho la vyama vya wafanya kazi DGB. Haya yote yanashuhudia jinsi hali ilivyozidi kuwa ya kutatanisha, ambayo inabidi kutafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la kusini mwa Ujerumajni SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, kuhusu mada hii: Wafanya kazi katika viwanda vya kutengeneza magari vya Glivice nchini Poland pamoja na wa Azambuja nchini Ureno, ndio wanaonufaika hasa na mpango huu wa mageuzi wa General-Motors. Kwa mkakati wake vitafanyiwa marekebisho tu viwanda vya zile nchi zilizo na masoko ya kuuza magari yao na ambazo haziumizwi sana na tatizo la ukosefu wa ajira. Hali hizi mbili hazikutikani katika Ujerumani. Kwa sababu hii inavibidi vyama vya wafanya kazi kuelewa kwamba, Ujerumanji si kisiwa na kwamba, mikakati yao ya miaka ya sabini na ya themanini, ilikwishapitwa na wakati.