Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
21 Oktoba 2004Gazeti la mashariki mwa Ujerumani LEIPZIGER VOLKSZEITUNG, kuhusu
kumalizika mgomo wa wafanya kazi wa kampuni la magari chama ya Opel katika Ujerumani, linaandika: Mgomo wao ulikuwa ni muhimu sana, kwa sababu umepelekea kampuni hilo kuanza tena na utengenezaji wa kawaida. Kwa mgomo wao wafanya kazi walionyesha jinsi mzozo, mageuzi na upunguzaji masaa ya kazi zinavyokabiliwa na hatima sawa. Yule anayepigana kwa ajili ya kampuni lake, anabidi pia kuonyesha utayarifu wa kulitumikia.
Nalo gazeti la mji wa Würzburg TAGESPOST, linachangia mada hii kwa kuandika: Wafanya kazi wa kampuni la Opel, hawakwenda kuandamana barabarani, kwa ajili ya kujaribu kufanya mapinduzi, bali walinuwia kuhakikishiwa haki zao. Mgomo wao uliwambinya viongozi kutangaza hatimaye ni viwanda gani ambavyo huenda vikafungwa na vipi viweze kuendelea na kazi kama kawaida. Kila mmilikaji kiwanda mwerevu anajua umuhimu wa wafanya kazi waaminifu. Kupatikana mhanga katika nyakati mbaya, ni bora kuliko kwenda kutafuta mikopo ya benki.
Gazeti la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU kuhusu mada hii linaandika: Kuvunjwa kwa mgomo huu, hakumaanishi kamwe wafanya kazi wameshindwa, bali kinyume chake kunashuhudia namna wafanya kazi wanavyochukua hatua kwa busara. Lakini shirika la magari la kimarekani General-Motors, lisije likafurahi mapema. Ikiwa shirika hili litajaribu kuwakandamiza wafanya kazi wakati majadiliano yakiendelea hapa shaka wafanya kazi watarejea barabarani kujihami kwa machungu zaidi.
Nalo gazeti la kaskazini NRODSEE ZEITUNG linatoa shauri kwa kuandika: wawakilishi wa wafanya kazi wangeshauriwa vizuri iwapo wangechukua hatua za moja kwa moja za dharura, ili kupata ukweli wa wapi kampuni linapata faida na wapi linakumbwa na hasara.
Gazeti la HEILBRONNER STIMME, kuhusu tangazo la tume ya jumuiya ya ulaya la kuishtaki Ujerumani kwenye mahakama ya ulaya kujibu ni kwa sababu gani haitekelezi ipasavyo mapatano ya kibiashara ya posta na vikopo vya vinnywaji, linakumbusha: Zinabakia siku chache tu kabla ya Ujerumani kuweza kuvuta tena pumzi. Kwani tarehe 31 oktoba tume ya jumuiya ya ulaya itavua madaraka yake pamoja na kamishina wake Frits Bolkenstein. Tangu miaka kamishina huyu kutoka Uholanzi, anapigania soko huru la ndani. Harakati muhimu, lakini baadhi ya nyakati anakwenda mbali sana. Katika harakati zake Bolkenstein mara nyingi anaonekana kutaka kuichukulia hatua Ujerumani makusudi. Katika mashtaka yake anatumia sana urasimu mwingi.
Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la biashara HANDESBLATT, kuhusu mada hii: Tume ya jumuiya ya ulaya hususan kamishina wa mashindano Mario Monti, kwa kweli walichangia mengi mnamo miaka iliyopita. Katika tangazo hili jipya la mashtaka, pia wanabidi kutoa mchango wa kulipinga, kwa sababu katika uchumi wa umma wa Ujerumani, panakutikana hali ya mashindano, hasa pale ambapo mashirika pamoja na wanasiasa walijaribu kuyazuwia. Pia wakati ujao Ujerumani itahitaji mkaguzi wake mjini Brussels, wa kusimamia namna inavyotekeleza masharti ya pamoja ya biashara.