Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani hii leo
18 Agosti 2005Kuhusu timu ya „wenye ujuzi“ gazeti la KIELER NACHRICHTEN limeandika:
„Anaweza kushusha pumzi kidogo Angela Merkel.Timu yake ya wajuzi,imeshaundwa baada ya wiki kadhaa za mkorogano zinapohusika mada za uchumi na mazingira-Edmund Stoiber hajapanda jukwaani kumdhihaki mwenyekiti wa CDU na nyota ya timu hiyo KIRCHOF aling’ara ajabu alipojitokeza rasmi kwa mara ya kwanza hadharani.
Kishindo kikubwa kinachomkabili Merkel kinasababishwa na wanasiasa wanaume ambao jana hawajakuwepo jukwaani.Kwamba mabwana Seehofer,Merz,Koch na Wulff wanakaa kimya,kwasababu hii au ile,hadi uchaguzi utakapoitishwa,ni bora zaidi kwa mtetezi huyo wa kiti cha kansela.“
Gazeti la mjini Würzburg-TAGESPOST limeandika:
„Baada ya kutangazwa hadharani timu ya wenye ujuzi,mmoja anaonyesha kuwavutia watu zaidi: PAUL KIRCHOF.Mshutuko kama huo wa kusisimua ulihitajika ili kuchangamsha kampeni ya uchaguzi ya CDU/CSU ambayo hadi wakati huu ilikua ya kubabaisha babaisha.Yeyote aliyegundua nini kiko nyuma ya karata hizo za bibi Merkel,hajakawia kuungama pia,aliyeng’ara zaidi si mwengine isipokua yule ambae si mfuasi wa chama chochote,mtaalam wa masuala ya kodi ambae hadi wakati huu CDU/CSU hawakua nae.“
Gazeti la mjini Rostock,Die OSTSEE-ZEITUNG linajiuliza:
„Paul KIRCHOF ni nani?“ na jibu linafuata hapo hapo :Mtu huyo mpya katika kundi la Merkel,amewashtuwa wengi.Mtaalam huyo wa kiuchumi na mwenye ujuzi,,hakimu wa zamani wa korti kuu ya katiba,ambae si mfuasi wa chama chochote kile,msomi na mwanasiasa asiyechelea kusema akifikiricho ni jaza kwa timu ya wenye ujuzi ya mpinzani wa Schröder katika uchaguzi mkuu ujao.“
Gazeti la RHEIN-NECKER-ZEITUNG la mjini Heidelberg linahisi:
„Mmoja tuu alisimama sipo kidogo jana katika picha ya timu ya Merkel-kwa maneno mengine hakuhusika na wenye ujuzi-Edmund Stoiber.Muhimu kwake,na hasa mtu akizingatia yaliyotokea kabla,muhumi kwake kwa hivyo ilikua kuitumia fursa hiyo kubainisha pamoja na mtetezi wa CDU/CSU,upepo unavuma upande gani.“
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linazungumzia hitilafu za maoni ndani ya vyama ndugu vya CDU/CSU na kuhoji:
„Mtetezi huyo wa kike anakabwa na kishindo cha kutaka kubadilisha haraka haraka mambo chungu nzima.Hata waliokinai wa magharibi wanabidi nao pia wajiambatanishe hivi sasa na hali jumla ya utandawazi na hakuna asilani njia ya kuubadilisha mfumo huo.Na Edmund Stoiber,nae pia anatambua hatari ya matokeo ya sera kama hizo hata kwa chama chake cha CSU katika jimbo la Bavaria.“
Gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE la mjini Erfurt linajishughulisha zaidi na uamuzi wa bibi Merkel wa kuwateuwa wataalam hao.Gazeti linaandika:
„Jaji wa zamani na mtaalam wa kodi ya mapato PUL KIRCHOF ,ndie hasa aliyetia fora katika timu hiyo ya wenye ujuzi iliyotangazwa jana na bibi Angela MERKEL:Hata hivyo mtu akitilia maanani viroja vya kisiasa mjini Berlin,basi hata nuru ya Professor huyo haitaacha kufifia.Hoja zake kali na msimamo wake shupavu kuhusu masuala ya kiuchumi,imeacha madowa.Na hakuna uhakika kama kansela wa kike atatia njiani sera kama hizo.Na miongoni mwa wapiga kura si wengi pia wanaomjua.“
Gazeti la FRANKFURT NEUE PRESSE limezungumzia juu ya kuuliwa muasisi wa jumuia ya watawa wa TAIZE, na kuandika:
„Frère Roger ,maishani mwake alikua akipigania amani na upendo miongoni mwa jamii.Kwamba yeye ndie anaeangukia mhanga wa shambulio la kikatili,hakuna ambae hajaingiwa na hofu.Polisi wanahisi ni rahisi,ukizingatia hali namna ilivyo wakati huu wa siku ya vijana wa dunia, kupitisha hatua kali kali dhidi ya mashambulio ya kigaidi kuliko kujikinga dhidi ya wenye kichaa.Kwasababu shambulio kama hili halikadiriki.Ili kuhakikisha usalama wa kiongozi mkuu wa kanisa katoliki ulimwenguni Benedikt wa 16,aliyewasili mjini Cologne hii leo,hatua za usalama zimeimarishwa.Kinyume na Frère Roger,walinzi kadhaa wataandamana nae.Lakini ulinzi wa mia bin mia hakuna anaeweza kuudhamini."