Uchaguzi Ujerumani: CDU/CSU waongoza matokeo ya awali
23 Februari 2025Matokeo ya awali kutoka uchaguzi wa Ujerumani wa 2025 yametoka, yakionyesha kwamba Muungano wa vyama vya mrengo wa wastani wa kulia vinaongoza kwa asilimia 28 vikifuatiwa na chama cha mrengo mkali cha AfD kilicho na zaidi ya asilimia 20. Chama tawala cha SPD kilikuw akatika nafasi ya tatu, kwa asilimia 16.3, mbele ya washiriamwao wa sasa serikali, chama cha watetezi wa Mazingira, die Grüne, kilicho na asilimia 12.3.
Habeck: 'Merz anapaswa kuanza kujichukulia kama ukansela, siyo mgombea wa jimbo'
Mgombea mkuu wa Chama cha Kijani, Robert Habeck, ametetea matokeo ya chama chake ya asilimia 13 ya kura akiyaita "ya heshima," na kueleza kuwa chama hicho cha Kijani "hakijaanguka" kama vyama vingine vya serikali ya mseto vya SPD na FDP.
Hata hivyo, amelaumu matokeo duni ya chama chake kwa mwenendo wa Friedrich Merz wa CDU, akisema kuwa amechochea "msimamo mkali" kwa kiasi kikubwa.
Habeck, ambaye amehudumu kama makamu wa kansela tangu 2021, alikuwa akizungumzia jaribio la utata la Merz la kupitisha hoja bungeni kwa msaada wa chama cha mrengo mkali wa kulia, AfD, hatua iliyosababisha baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa kushoto na kushoto-kati kudai vyama visishirikiane na CDU.
"Sikuweza kutoa ahadi hiyo," alisema Habeck. "Nimesema kila mara kuwa tunataka kubeba majukumu, kwa hivyo njia hiyo haikuwa wazi kwetu. Na tumelipa gharama yake."
Kambi ya kihafidhina ya Merz, hususan Waziri Mkuu wa Bavaria, Markus Söder, imekataa kushirikiana na Chama cha Kijani, lakini Habeck amesisitiza kuwa yuko tayari kwa mazungumzo—mradi tu Merz abadili mwenendo wake.
Usiku wa kuamkia uchaguzi, Merz alitoa hotuba kali kwa wafuasi wake akipaza sauti kwamba hakuna tena nafasi kwa "siasa za mrengo wa kushoto" au "sera za Kijani," jambo ambalo Habeck aliliona kuwa halikufaa.
"Merz sasa ana mamlaka ya kuunda serikali na natumai atatambua uzito wa jukumu alilo nalo," alikiambia kipindi cha habari cha Tagesschau. "Mrengo wa kati umedhoofishwa, na Merz anapaswa kujiuliza ikiwa amechangia hilo. Anapaswa kuanza kuonyesha uongozi wa ukansela, si kama mgombea wa kampeni za jimbo."
Merz wa CDU/CSU asifu ‘usiku wa kihistoria wa uchaguzi’
Kiongozi wa chama cha CDU Friedrich Merz amewahutubia wafuasi katika makao makuu yachama katika kile alichokiita "usiku wa kihistoria wa uchaguzi" kwa muungano wake wa kihafidhina.
"Sisi, CDU na CSU,vyama vy amuungano, tumeshinda uchaguzi huu," alisema Merz, akifuatiwa na makofi marefu kutoka kwa wafuasi waliokusanyika kwa wingi.
"Tumeshinda kwa sababu CDU na CSU zilifanya kazi kwa pamoja kwa ufanisi mkubwa na zilijiandaa vyema kwa uchaguzi huu," aliongeza Merz, akimshukuru kiongozi wa CSU, Markus Söder, aliyesimama kando yake wakati wa hotuba, kwa mchango wake katika kampeni. Merz pia amelishukuru kundi la vijana wa chama, Junge Union, kwa ushiriki wao katika kampeni.
Soma pia: Masuala ya uhamiaji yatawala kampeni za uchanguzi Ujerumani
"Asanteni kwa kuniamini," alisema Merz, ambaye ndiye mgombea anayeonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuchukua kiti cha ukansela. Aliongeza kuwa safari ya mbele haitakuwa rahisi.
"Dunia haitatusubiri, haitasubiri mazungumzo marefu ya kuunda serikali ya muungano. Tunapaswa kuwa tayari kuchukua hatua haraka, ili tufanye kile kilicho sahihi kwa Ujerumani, ili tuwepo tena Ulaya, na ili dunia ionyeshe kuwa Ujerumani ina serikali inayotegemewa tena," alisema Merz.
SPD: 'Kushindwa kwa kihistoria'
Katibu Mkuu wa SPD amempongeza Friedrich Merz na CDU huku akikiri "kushindwa kwa kihistoria" kwa chama chake.
"Hii ni kushindwa kwa kihistoria, jioni yenye uchungu kweli," alisema Matthias Miersch katika mazungumzo na shirika la utangazaji la umma ARD, baada ya SPD kutabiriwa kupata takriban asilimia 16 pekee ya kura.
"Ni wazi kuwa uchaguzi huu haukupotezwa katika wiki nane zilizopita tu," alifafanua. "Muungano umekuwa ukipitia mawimbi makali kwa miaka kadhaa, na sasa umeondolewa madarakani kupitia sanduku la kura. Ni serikali ya aina gani itakayoundwa sasa, na kwa kiwango gani SPD inaweza au inapaswa kuchukua majukumu ya serikali, hatuwezi kusema kwa sasa. Merz ana mamlaka ya kuunda serikali, na tutalazimika kusubiri kuona uwezekano wa miungano mbalimbali."
Soma pia: Umaarufu wa vyama vikubwa Ujerumani washuka kidogo
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa Kansela wa SPD anayemaliza muda wake, Olaf Scholz, Miersch alisema: "Tulikuwa na kansela aliyeliongoza taifa hili kupitia nyakati ngumu, lakini mwishowe hakuweza kuwashawishi wapiga kura. Hilo ni jambo halisi katika usiku huu wa kuvunja moyo."
AfD yasifu matokeo ya uchaguzi kuwa ya 'kihistoria'
Vyombo vya habari vinadhibitiwa vikali kwenye sherehe ya usiku wa uchaguzi ya AfD, lakini niliweza kumuuliza mmoja wa wanachama wa zamani na wa mwanzo kabisa wa AfD, Albrecht Glaser, maoni yake kuhusu matokeo.
"Kuwa mbele ya SPD, chama cha siasa kongwe zaidi nchini Ujerumani, ni jambo la kihistoria," aliiambia DW. "Na wao (SPD) hawajaelewa kwa nini hali iko hivyo."
Hata hivyo, ninalazimika kusema kuwa mwitikio wa awali ndani ya ukumbi baada ya matokeo ya awali kutangazwa ulikuwa wa chini mno. Hii inaonyesha umbali ambao chama kimefika. Wengi ndani ya AfD walikuwa na matumaini ya kufikisha angalau zaidi ya asilimia 20 kwa urahisi. Hilo huenda bado likatokea, lakini itakuwa usiku mrefu. Vyovyote iwavyo, chama cha mrengo wa kulia cha AfD kimeandika historia usiku wa leo.