UAE yakanusha kupeleka silaha kwa RSF Sudan
9 Mei 2025Umoja wa Falme za Kiarabu umekanusha ripoti ya shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International inayoituhumu kwa kuwapelekea silaha zilizotengezwa China, wapiganaji wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces RSF nchini Sudan.
Naibu waziri anayeshughulikia masuala ya usalama na kijeshi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Salem Aljaberi amesema nchi yake inapinga pendekezo kwamba inapeleka silaha kwa upande wowote katika mzozo wa vita unaoendelea nchini Sudan.
Aljaberi amesema madai hayo hayana msingi wala ushahidi.
Jana Alhamisi shirika la Amnesty International lilisema limetambua mabomu ya China chapa GB50A na mitambo ya kuvurumishia makombora kwa kupitia uchambuzi wa video ya mashambulizi ya kikosi cha RSF katika mji wa Khartoum na Darfur.
Shirika la Amnesty International limesema Umoja wa Falme za Kiarabu ndiyo nchi pekee iliyoagiza mitambo hiyo kutoka China katika mkataba wa mwaka 2019.