Tunisia yafunga kambi kubwa za wakimbizi
5 Aprili 2025Msemaji wa kikosi cha ulinzi wa kitaifa, Houcem Eddine Jebabli, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba takriban wahamiaji 20,000 walikuwa wamejenga mahema katika maeneo ya mashamba katika mikoa ya mashariki ya El Amra na Jebeniana.
Jebabli amesema kiasi cha watu 4,000 wa mataifa mbali mbali walikuwa wameondoka kwenye kambi moja iliyovunjwa na mamlaka, na kwamba operesheni hiyo itaendelea katika siku zijazo.
Wanawake wajawazito na wagonjwa wanashughulikiwa na mamlaka
Jebabli, ameongeza kuwa baadhi ya wahamiaji walitawanyika katika maeneo hayo ya mashambani, huku wanawake wajawazito na wagonjwa wakishughulikiwa na mamlaka ya afya.
Amesema lilikuwa jukumu lao kukabiliana na hali hiyo ya wahamiaji.
Kambi hizo ziliibua hasira kutoka kwa wakaazi katika vijiji vya karibu, na kusababisha shinikizo dhidi ya mamlaka.