Wafghanistani walio hatarini waisihi Ujerumani kuwapa visa
2 Septemba 2025Kundi la takriban Wafghanistani 200 walioko hatarini kutokana na vitisho vya Taliban limeandika barua kwa Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, wakiomba waruhusiwe kuhamia Ujerumani.
Barua hiyo, ambayo shirika la habari la dpa liliiona Jumanne, inatoa onyo kali kuhusu "msongo wa kisaikolojia usiovumilika” kutokana na "hofu ya kudumu ya uvamizi wa Taliban, kisasi, kukamatwa kiholela, utekaji, mateso au hata kifo.”
Baada ya Taliban kurejea madarakani mwaka 2021, serikali ya Ujerumani ilianzisha mpango wa kuwahamisha wafanyakazi wa zamani wa taasisi za Kijerumani na familia zao.
Berlin pia iliahidi kuwapa hifadhi Wafghanistani wengine walioko hatarini, wakiwemo mawakili, wanahabari na watetezi wa haki za binadamu.
Hata hivyo, tangu Mei mwaka huu, serikali ya Merz imeisitisha kwa muda mipango ya kuwapokea mamia ya Wafghanistani waliokuwa wamejumuishwa kwenye mpango wa "admission programme”, ikisema inalenga kupunguza idadi ya wahamiaji.
Hatua hiyo imekuwa na athari kubwa, hasa baada ya serikali ya Pakistan kuanza kuwarejesha nchini Afghanistan wale waliokuwa wakisubiri safari ya kuelekea Ujerumani.
'Kila saa ya uchelewaji inaweza kugeuka hukumu y akifo'
Miongoni mwa waliotia saini barua hiyo ni wasanii, majaji, waendesha mashtaka, watumishi wa umma, wanawake wanaoongoza kaya na wanahabari.
Kwa sasa, wanahifadhiwa kwenye nyumba salama jijini Kabul na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Ujerumani (GIZ), lakini wanasema kila saa ya kuchelewa kwa msaada inaweza kugeuka kuwa hukumu ya kifo kwao.
"Tuliamini ahadi zenu. Tafadhali msiruhusu imani hii kutugharimu maisha yetu — na ya watoto wetu,” barua hiyo ilisomeka.
Hata hivyo, ingawa mahakama ya Ujerumani iliamua Jumatatu kwamba Berlin ina haki ya kusitisha utoaji wa visa katika baadhi ya kesi, baadhi ya Wafghanistani wamefanikiwa kupata nafasi ya kuhamia Ujerumani kupitia kesi za mahakamani.
Jumatatu hii, ndege ya kibiashara kutoka Istanbul iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Hanover ikiwa na raia 45 wa Afghanistan waliopatiwa visa na kukamilisha ukaguzi wa usalama, huku wengine wawili wakithibitishwa kuwasili baadaye.
Chanzo: DPA