Tshisekedi atakiwa kuzingatia maslahi ya taifa lake
29 Aprili 2025Tamko la nia ya amani lililosainiwa kati ya Kongo na Rwanda mjini Washington Ijumaa iliyopita chini ya uangalizi wa serikali ya Marekani kwa nia ya makubaliano ya amani linatazamwa vibaya na upinzani wa kisiasa nchini Kongo.
Upinzani wamshtumu Tshisekedi kwa kujitetea kimaslahi
Muungano wa vyama vya upinzani wa Lamuka chini ya uongozi wa Martin Fayulu umemtuhumu Rais Tshisekedi kwa kuweka rehani madini ya Kongo ili kulinda maslahi yake ya kisiasa.
Kwa mujibu wa msemaji wa muungano huo, Prince Epenge, makubaliano kati ya Kongo na Rwandakwa nia ya kiuchumi kama inavyotakiwa na Marekani katika eneo la Maziwa Makuu yatasababisha makampuni ya Marekani kuja nchini Rwanda ambayo ina viwanda, na kutengeneza nafasi za ajira huko, huku Kongo ikiwa shimo ambalo malighafi inachimbwa tu.
Shinikizo la kimataifa laongezeka dhidi ya Rwanda na waasi wa M23
Hata hivyo, Prince Epenge amesema Lamuka inaunga mkono mazungumzo na makubaliano mengine yoyote kwa jina la amani, lakini isiwe kwa njia ya msongamano, kama inavyoonekana wakati huu.
Marekani yadaiwa kutumia makubaliano kwa uporaji
Kwa upande wake, chama cha siasa cha PPRD cha rais wa zamani, Joseph Kabila, kinaona makubaliano haya kama kitendo cha uporaji kinachoungwa mkono na Marekani. Chama hicho kinamshuku Rais Tshisekedi kwa kutaka kukabidhi migodi ya Kongo kwa jirani yake Rwanda.
Kwa upande wao, wapinzani Seth Kikuni na Claudel Lubaya wanakosoa mijadala iliyofanyika katika miji ya Doha nchini Qatar, na Washington nchini Marekani, wakikemea kile wanachokiita kuwa kipaumbele kinachotolewa kwa masuala ya kiuchumi pekee.
Asasi za kiraia zataka mazungumzo ya kikanda
Lakini pia, asasi mbalimbali za kiraia zimetoa wito wa kufunguliwa kwa mazungumzo ya kikanda yanayozijumuisha nchi zote jirani za Kongo, ikiwa ni pamoja na Rwanda.
Masharti katika hati ya wakuu wa diplomasia wa Kongo na Rwanda
Hati iliyotiwa saini hivi karibuni kati ya wakuu wa diplomasia za Kongo na Rwanda inasisitiza, hasa, juu ya heshima ya uhuru na mamlaka ya mipaka ya kila taifa.
Pia inasisitiza kuondolewa kwa vikosi vya Rwandakutoka katika maeneo wanayoyakalia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako wanaliunga mkono kikamilifu kundi la waasi wa M23/AFC mashariki mwa Kongo.
Qatar inaunga mkono juhudi za amani kwa Kongo
Akizungumza na ujumbe wa maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kiprotestanti wa CENCO-ECC Jumatatu mjini Doha, Qatar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulaziz bin Saleh Al-Khulaifi, alithibitisha kwamba Qatar inaunga mkono juhudi zinazofanywa kuleta amani Kongo.