Tshisekedi asema Kongo iko tayari kwa mkataba na Marekani
20 Machi 2025Akizungumza na kituo cha televisheni cha Fox News, Tshisekedi amesema makubaliano ya aina hiyo yataiwezesha Congo kuchimba madini yake kupitia kampuni za Marekani huku yenyewe ikinufaika kwa kuimarisha mifumo yake ya ulinzi na usalama.
Soma pia: Kwanini Rwanda na Ubelgiji zimekata uhusiano wa kidiplomasia?
Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini ikiwemo kobalti na urani imekuwa inapambana kundi la waasi wa M23 linaloungwa mkono na Rwanda ambalo limefanikiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu kuchukua udhibiti wa maeneo makubwa upande wa mashariki mwa nchi hiyo.
Hapo jana kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi na kuingia mji mdogo wenye utajiri wa madini wa Walikale licha ya mwito wa kusitishwa mapigano uliotolewa na Rais Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame walipokutana nchini Qatar mapema wiki hii.