Trump: Zelensky yuko tayari kwa mazungumzo na Urusi
5 Machi 2025Hayo yanajiri wakati ambapo Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amependekeza kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine.
Akilihutubia Bunge la Marekani kwa mara ya kwanza baada ya kurejea katika Ikulu ya Marekani, White House, Trump amedai kuwa anafanya kazi bila kuchoka kuumaliza mzozo mbaya wa Ukraine. Kulingana na Trump, Marekani imeipatia Ukraine msaada wa kijeshi wenye thamani ya mamia ya mabilioni ya dola za Kimarekani.
''Mamilioni ya Waukraine na Warusi wameuawa au kujeruhiwa bila sababu katika mzozo huu wa kutisha na wa kikatili, usio na mwisho. Marekani imepeleka mabilioni ya dola kusaidia katika ulinzi wa Ukraine, bila dhamana yoyote.''
Trump pia aliisoma barua aliyotumiwa hivi karibuni na Rais Zelensky. Akiisoma barua hiyo mbele ya Bunge, Trump alisema Ukraine iko tayari kwenda kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo ili kuleta amani ya kudumu karibu, na kwamba hakuna anayetaka amani zaidi ya Waukraine.
Ukraine yasema iko tayari kusaini makubaliano ya madini
Kuhusu makubaliano ya madini na usalama, Trump amesema barua hiyo ya Zelensky imefafanua kuwa Ukraine iko tayari kusaini makubaliano hayo muda wowote ule. Katika barua hiyo Zelensky alibainisha kuwa wanathamini sana kile ambacho Marekani imekifanya kwa ajili ya kuisaidia Ukraine.
Soma pia:Ukraine yasema inao uwezo wa kuendelea kupambana na Urusi
Kwa upande wake Rais Zelensky amesisitiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi yake na Marekani. Akizungumza jana jioni, Rais Zelensky amesema ingawa Ukraine inaweza kujitetea yenyewe, kwa upande wao, uhusiano wa kawaida wa ushirikiano na Marekani ni muhimu katika kuvimaliza vita.
Wakati huo huo, Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amependekeza kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine ambayo yanaweza kuwahusisha maafisa wa Marekani. Katika mahojiano yaliyorekodiwa Februari 27 na kuchapishwa leo, Lukashenko amesema kwamba Trump alikuwa amefuata sera mahiri ya kigeni.
soma pia: Ukraine yahimiza dhamana ya usalama kabla ya mpango wa amani
Lukashenko ni mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin, na nchi yake imewekewa vikwazo na Marekani na Ulaya kutokana na kuunga mkono shughuli za kijeshi za Urusi nchini Ukraine, na hatua ya serikali yake kuukandamiza upinzani.
Ama kwa upande mwingine, Ufaransa imesema kwamba inafanya juhudi za kurekebisha uhusiano kati ya Ukraine na Marekani ili kupata amani ya kudumu na imara. Ufaransa na Uingereza zimependekeza makubaliano ya muda kati ya Urusi na Ukraine kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia za Ulaya zilizoanzishwa ili kupata uungaji mkono wa mataifa ya Magharibi kwa Ukraine baada ya kuibuka tofauti kati ya Trump na Zelensky.