Trump, Zelensky warushiana maneno hadharani
1 Machi 2025Trump aliyeonya kwamba Ukraine haiwezi kukabiliana na Urusi bila ya msaada wa Marekani, alidai kwamba Rais Vladimir Putin yuko tayari kwa mkataba wa amani.
Marekani ilikuwa imetarajia kusaini makubaliano ya kibiashara ambayo yangeliiwezesha kupata madini adimu kutoka Kiev, huku pia ikitumia fursa hiyo kumshinikiza Zelensky akubali kusitisha mapigano na Urusi.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Ukraine alijibizana na Trump na makamu wake, JD Vance, juu ya ulazima wa kwanza kupatiwa hakikisho la ulinzi kutoka Washington endapo Putin atakiuka makubaliano hayo.
Soma zaidi: Viongozi wa Ulaya waafikiana kuhusu kuimarisha usalama wao
Viongozi kadhaa wa Ulaya, Amerika Kaskazini na Australia wameonesha uungaji wao kwa Ukraine, baada ya kile kilichotajwa kama mkutano wa kudhalilishana kati ya Trump na mgeni wake katika Ikulu ya White House.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambaye mwanzoni mwa wiki hii alikuwa Washington kukutana na Trump, amesema ni Ukraine ndiyo iliyovamiwa na si kinyume chake.
Australia imesema itaendelea kusimama na Ukraine, huku Umoja wa Ulaya, kupitia rais wake, Ursula von der Leyen, ukimpongeza Zelensky kwa kusimama imara kutetea heshima ya nchi yake.