Trump: Zelenskiy yuko tayari kuipa Urusi Crimea
28 Aprili 2025Haya yanafanyika wakati mazungumzo ya kusaka amani yakiingia kile Washington ilichokiita wiki muhimu.
Trump ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bedminster, New Jersey, alipoulizwa kama alifikiri Zelensky alikuwa tayari kubadili msimamo wake kuhusu Urusi kuikalia Crimea ikiwa ni moja ya sharti alilopewa ili kuhitimisha mzozo wa muda mrefu kati ya Urisi na Ukraine.
"Nadhani ni hivyo”, alijibu kwa ufupi Trump mara baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma ya Ukraine kuikabidhi Crimea kwa Urusi.
Mashambulizi baada ya mazungumzo ya Vatican
Mbali na kuaimini kuwa Ukraine itakubaliana na shinikizo la Washington, Trump pia amezidisha shinikizo kwa kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi akimtaka kuacha kufyatua risasi na badala yake asaini makubaliano ya kumaliza vita hivyo vilivyoanza na uvamizi wa Moscow mnamo mwezi Februari 2022.
Urusi ilianzisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora usiku baada ya mazungumzo ya Vatican, na kuua watu wanne katika mikoa ya mashariki mwa Ukraine na kujeruhi zaidi ya dazeni.
"Namtaka aache kufyatua risasi, aketi chini, na kutia saini mkataba," alisema Trump hiyo jana Jumapili alipoulizwa anataka nini kutoka kwa Putin. "Tuna vikwazo vya mkataba, naamini, na nataka asaini." Ameongeza Trump.
Nayo Ukraine hapo Jumapili ilifanya shambulizi kubwa la ndege zisizo na rubani katika eneo la Brynsk huko Urusi na kuua raia mmoja na kumjeruhi mwingine.
Washington bado haijaweka wazi mpango wake wa amani lakini imekuwa ikisisitiza kutambuliwa kwa Crimea kama sehemu ya Urusi, hali ambayo Ukraine imekuwa ikigoma kama njia ya kumaliza mzozo huo.
Korea Kaskazini yapeleka wanajeshi Urusi
Wakati hayo yakijiri, Rais Putin amemshukuru kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, kufuatia majeshi ya nchi hiyo kufanikisha kulirejesha eneo na Kursk la Urusi lililokuwa kwenye himaya ya majeshi ya Ukraine.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Korea ya Kaskazini la KCNA, Pyongyang ilipeleka wanajeshi takribani elfu 10 kuukombioa mji huo tukio ambalo Rais Putin ameliita kuwa la kirafiki kati ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo ya kusaka amani kati ya Urusi na Ukraine yanatajwa kuingia katika wiki muhimu kufuatia kukwama wiki iliyopita.
Katika awamu ya sasa, mazungumzo hayo yanatarajiwa kuwakutanisha washirika wa Urusi, Ukraine na Marekani.