Trump atangaza kupandisha ushuru kwa kati ya 15-20%
28 Julai 2025Rais Trump amesema hayo akiwa mjini Turnberry, Scotland akizilenga nchi ambazo hazifanikiwa kuingia makubaliano ya kibiashara na Marekani.
"Ningesema itakuwa kati ya asilimia 15 hadi 20," Trump aliwaambia waandishi wa habari, akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer katika kituo chake cha gofu huko Turnberry, Scotland. "Pengine ni kati ya namba hizi mbili."
Trump amesema serikali yake itatuma barua hivi karibuni kwa mataifa karibu 200 na kuyafahamisha kuhusiana na kiwango hicho cha ushuru wa mauzo ya bidhaa nchini Marekani.
Trump alitangaza kuyapandishia ushuru wa asilimia 10 mataifa mengi kuanzia mwezi Aprili huku mengine yakisubiri ongezeko hili kuanza kufanya kazi Agosti 1, 2025.
Trump akosolewa kwa kuchanganya urais na biashara
Trump aidha amekutana na Starmer kuangazia upya makubaliano ya kibiashara baina ya mataifa hayo mawili waliyoyasaini mwezi uliopita, lakini pia waligusia suala la Gaza wakisema Israel ina jukumu kubwa kuhusiana na kile kinachotokea Gaza.
Mwishoni mwa wiki, Trump alitembelea viwanja vyake vya gofu wakati familia yake ikijiandaa kufungua viwanja vingine nchini Scotland mnamo mwezi Agosti.
Wakosoaji wanasema kwamba ziara hiyo ya nje, aliyoambatana na rundo la washauri wake, watumishi wa Ikulu ya White House, Usalama wa Taifa na waandishi wa habari, ni mfano tosha wa namna Trump anavyochanganya majukumu yake ya urais na kupigia debe maslahi yake ya kibiashara.
Lakini White House imeiita ziara hiyo kuwa ni ya kikazi.