Trump: Ukraine itaamua kivyake mipaka yake
15 Agosti 2025Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatajadiliana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwa niaba ya Ukraine, bali ataiacha Ukraine kujiamulia kivyake mjadala wa kuachia sehemu ya ardhi yake kwa Urusi. Trump amesema hayo kuelekea mkutano wake wa kilele na Putin kule Alaska kwa lengo la kusaka amani ya Ukraine.
Rais Trump amesema lengo lake lilikuwa kuanzisha mazungumzo kati ya pande mbili husika Urusi na Ukrain huku masuala ya kubadilishana maeneo yakitarajiwa kujadiliwa wakati huo.
"Yatajadiliwa, lakini nitaiachia Ukraine kufanya uamuzi huo na nadhani watafanya uamuzi sahihi. Lakini sipo hapa kujadiliana kwa niaba ya Ukraine. Nipo hapa kuwaleta pamoja mezani kwa mazungumzo,'' Trump aliwaambia waandishi habari akiwa kwenye ndege yake.
Kauli ya Trump huenda ikatoa uhakikisho kidogo kwa Ukraine, inayohofia kwamba mazungumzo kati ya Marekani na Urusi yanaweza kuwa na makubaliano ya kumaliza machafuko lakini kwa gharama ya Ukraine.
Trump: Mashambulizi ya Urusi ni mbinu ya kujiandaa kwa mazungumzo
Trump amesema huenda mashambulizi ya Urusi yanalenga kumpa Putin nguvu katika mazungumzo yoyote ya kumaliza vita hivyo.
‘'Ninadhani wanajaribu kuzungumza. Anajaribu kujiandaa. Akilini mwake, mashambulizi hayo yatamsaidia kupata mkataba mzuri. Hakika yanamuumiza lakini akilini mwake, atapata mkataba mzuri wakiendelea kuua.''
Rais Trump amesema anatarajia mkutano wake na Putin utakuwa na tija ikizingatiwa hali ilivyo na unyonge wa Uchumi wa Urusi.
Japo kwenye ujumbe wa Putin kuna wafanya biashara, Trump amesema hiyo ni ishara nzuri kwamba Urusi inataka kufanya biashara, lakini amesisitiza hakutakuwa na mikataba yoyote ya kibiashara hadi vita vimalizwe.
Mkutano huo wa ana kwa ana utafanyika katika kambi ya kijeshi huko Anchorage saa sita usiku majira ya Afrika Mashariki. Itakuwa mara ya kwanza kwa Putin kufika Marekani tangu alipoivamia Ukraine Februari 2022. Vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu kwa maelfu ya watu huku Urusi ikinyakua baadhi ya maeneo ya Ukraine.
Makubaliano yanaweza kuwa gharama kubwa kwa Ukraine
Miongoni mwa hofu kubwa ya Ukraine na Ulayakuhusu mazungumzo hayo ni kwamba huenda wakakubaliana kwamba Ukraine isalimishe baadhi ya maeneo yake kwa Urusi. Jambo ambalo Ukraine na washirika wake wa Ulaya wanapinga.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz aliyekutana na Zelensky wiki hii, amesema Rais Putin atakuwa na nafasi ya kukubali kumaliza vita nchini Ukraine atakapokutana na Trump. Na kwamba masuala ya mipaka ya maeneo yanaweza tu kuamuliwa kwa ridhaa ya upande wa Ukraine.
Kwa Putin, mkutano na Trump ni nafasi ambayo imetafutwa kwa muda mrefu ya kujadili makubaliano yanayoweza kuimarisha faida za Urusi, kuzuia juhudi za Ukraine kujiunga na jumuiya ya kijeshi ya NATO na hatimaye kuirudisha Ukraine upande wa Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye hatohudhuria mkutano wa kilele kati ya Marekani na Urusi huko Alaska, amesema anatarajia kupata taarifa kutoka kwa idara za ujasusi kuhusu mazungumzo hayo.
"Natarajia ripoti leo kutoka kwa idara zetu za ujasusi kuhusu nia ya sasa ya upande wa Urusi na maandalizi yao kwa mkutano wa Alaska," Zelensky aliandika hayo kwenye ukurasa wake wa Telegram.
Aliandika kuwa lengo kuu ni kuhakikisha mazungumzo kati ya Putin na Trump yanafungua njia ya mkutano wa pande tatu ambao utamjumuisha yeye pia.
"Ni wakati wa kumaliza vita, na Urusi lazima ichukue hatua stahiki. Tunategemea Marekani," alisema Zelensky.
(APTN, DPAE,RTRE)