Trump: Ukraine haikupaswa kuanzisha vita na Urusi
19 Februari 2025Hii leo Jumatano mjumbe wa Marekani anayehusika na maswala ya Ukraine amewasili mjini Kiyv. Na Urusi yaushambulia mji wa Odesa na kusababisha ukosefu wa umeme kwenye mji huo.
Mjumbe huyo wa Marekani anayeshughulikia maswala ya Ukraine Keith Kellogg, amewasili leo asubuhi katika mji mkuu wa Ukraine, Kiyv kwa mazungumzo na Rais Volodymyr Zelenskiy.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ameondoka kutoka Riyadh, Saudi Arabia hii leo Jumatano kuelekea Abu Dhabi, katika Falme za Kiarabu.
Alipokuwa katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riadh,Rubio aliuongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo na ujumbe wa Urusi ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov katika juhudi zinazolenga kusaidia mazungumzo ya amani ya Ukraine.
Soma pia:Russia, USA, zakubaliana kufikisha mwisho vita Ukraine
Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump amesema Ukraine haikupaswa kamwe kuanzisha vita na Urusi. Alipoulizwa na waandishi wa Habari kama ana ujumbe wowote kwa Ukraine ambayo huenda baada ya miaka mitatu ya mapigano, inahisi kuwa watu wake wamesalitiwa au wamekatishwa tamaa kwa kukosa kushirikishwa katika mazungumzo ya awali yaliyofanyika nchini Saudi Arabia.
Trump alipuuza madai hayo ya Ukraine ya kutojumuishwa katika mazungumzo kati ya Marekani na Urusi huko Saudi Arabia yanayolenga kuvimaliza vita Ukraine.
"Sawa, nadhani nimesikitishwa sana na kilichotokea nchini Ukraine. Nimeyaona haya kwa miaka mitatu. Ni vita ambavyo visingetokea kama ningekuwa rais kwa muda huo." Alisema.
Aliongeza kwamba "tumeshuhudia watu wakiuawa katika viwango ambavyo hatujawahi kuviona tangu vilipomalizika Vita vya Pili vya Dunia."
Aidha Trump aliongeza kwamba mzozo huo ungeliweza kutatuliwa kwa urahisi tangu miaka iliyopita.
"Lakini mimi nadhani nina uwezo wa kuvimaliza vita hivi."
Trump: Ukraine yakulaumiwa katika vita hivi
Donald Trump alionekana kupendekeza kuwa Ukraine ndio ingelaumiwa kwa vita vilivyoanza baada ya Urusi kuivamia nchi hiyo. Aliwaambia waandishi wa Habari katika makao yake ya Mar-a-Lago kwamba Ukraine imekuwa kwenye vita hivyo kwa miaka mitatu sasa na ndio ilitakiwa kuvimaliza hivyo.
Wakati hayo yanaendelea wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya leo Jumatano wamekubaliana awamu ya 16 ya vikwazo dhidi ya Urusi.
Vikwazo hivyo vinajumuisha marufuku ya kuagiza madini yanayotumiwa kutengeneza vyuma vya aluminium kutoka Urusi pamoja na kuzipiga marufuku meli zipatazo 73 zinazosafirisha bidhaa za nchi hiyo kwa kutumia bendera za nchi nyingine.
Soma pia:Marekani na Urusi waafikiana kuanzisha rasmi mchakato wa amani katika mzozo wa Ukraine
Huko mjini Paris Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anajiandaa hii leo Jumatano kwa duru nyingine ya mazungumzo na Umoja wa Ulaya na washirika wasio wa Ulaya kuhusu Ukraine katika nia ya kuratibu jibu la bara Ulaya kwa kile alichokiita "kitishio kilichopo" kutoka Urusi wakati ambapo kuna mabadiliko ya sera huko nchini Marekani.
Na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi imeshambulia mji wa Odesa ulio kusini mwa Ukraine.
Mashambulizi hayo ya usiku kucha yamesababisha kukosekana nguvu za umeme ambapo mamia ya watu wanakabiliwa na baridi kali. Zelensky amesema takriban wakazi 160,000 katika mji wa Odesa hawana umeme huku shule 13, shule moja ya chekechea na hospitali kadhaa zikikabiliwa na tatizo hilo la kukosa umeme.